Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio (katikati)
akiongea jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (wa kwanza kushoto) na wawekezaji wa Kampuni za
kutatifi na kuchimba mafuta na gesi nchini. Wa kwanza kulia ni
Mkurugenzi wa Utafiti wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC), Dkt. James Mataragio.
Baadhi ya Wawekezaji wa Kampuni
za kutafiti na kuchimba mafuta na gesi nchini, wakimsikiliza Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa
kikao chake na wawekezaji hao.
Baadhi ya Wawekezaji wa Kampuni
za kutafiti na kuchimba mafuta na gesi nchini, wakimsikiliza Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa
kikao chake na wawekezaji hao.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya
Dodsal, K. Surendran, akitoa taarifa ya utafiti kuhusu Kampuni hiyo
kugundua gesi eneo la Ruvu. Wengine wanaomsikiliza ni Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati). Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt.
Na Kalonga Kasati
Imeelezwa kuwa, Tanzania
inahitaji kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia rasilimali ya
Gesi asilia ambayo inatajwa kuwa chachu ya ongezeko la nishati ya umeme
jambo ambalo litachochea ukuaji wa viwanda nchini.
Hayo yalielezwa na Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akihitimisha vikao
vyake na wawekezaji wa makampuni yanayofanya shughuli za utafiti
na uchimbaji wa Mafuta na gesi nchini, na kuwataka wawekezaji hao
kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo kutokana mahitaji ya
nishati hiyo nchini.
Profesa Muhongo aliwaeleza
wawekezaji hao msimamo wa Serikali kuhusu nishati hiyo kuwa, Serikali ya
Awamu ya Tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda
vikubwa na vidogo huku rasilimali ya gesi asilia ikitajwa kuwa injini ya
kufikia malengo hayo na kuwataka kuhakikisha kuwa gesi inapatikana
nchini.
“Hatujagundua mafuta, lakini tuna
hazina kubwa ya gesi ambayo inawezesha kufikia malengo hayo. Ni lazima
kampuni hizi zibadili mwenendo wao wa namna ya kufanya kazi. Tunataka
kasi zaidi katika suala hili na kuhakikisha gesi inapatikana. Tunataka
umeme mwingi unaotokana na gesi, umeme nafuu na wa uhakika,”amesisitiza
Prof. Muhongo.
Aliongeza kuwa, Serikali imelenga
kujenga viwanda viwili vya Mbolea kutokana na gesi asilia na kuyataja
maeneo ambayo viwanda hivyo vitajengwa kuwa ni Kilwa Mkoani Lindi na
Mtwara.
Aidha, mbali na kutaja ujenzi wa
viwanda vya mbolea, alisema kuwa, mipango mingine ya Serikali ni kujenga
mitambo ya kusindika gesi ili pia Tanzania iweze kushindana na nchi
nyingine kusafirisha gesi iliyosindikwa nje ya nchi, jambo ambalo
litawezesha kupata fedha nyingi za kigeni.
“Tunataka kujenga mtambo wa
kusindika gesi asilia mkoani Lindi. Gharama za ujenzi huo zinatarajia
kufikia kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 30, utakuwa mradi mkubwa
zaidi na tayari eneo la ujenzi wa mtambo huo limepatikana,” amesema
Prof. Muhongo.
Pia alisema kuwa, mipango mingine
ni kutumia gesi majumbani ili kuachana na matumizi ya mkaa ambayo
yanatajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo,
na kuongeza kuwa, kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee matumizi ya mkaa kwa
siku moja yanafikia kiasi cha magunia elfu hamsini (50,000).
Vilevile, aliongeza kuwa, gesi
asilia ni kichochea kingine muhimu kitakachosaidia kuondokana na
umaskini na kuongeza pato la Taifa ikizingatia kuwa, ongezeko la
mahitaji ya kiuchumi linapanda kutokana na kuongezeka la idadi ya watu
wa kipato cha kati na kuongeza kuwa, “ tunataka Tanzania iondokane na
umaskini kupitia rasilimali za gesi na mafuta”.
Aidha, mbali na nishati ya gesi
asilia, Prof. Muhongo aliwaeleza wawekezaji hao kuwa, zipo rasilimali
nyingine ambazo wawekezaji wanaweza kuwekeza nchini na kuzitaja kuwa ni
nishati jadidifu, pamoja na vyanzo vingine vya upepo, mawimbi, umeme
wa jua na makaa ya mawe.
Katika hatua nyingine, Prof.
Muhongo aliwata wawekezaji hao kutoa taarifa za maendeleo ya
utekelezaji wa miradi yao ifikapo tarehe 1 Juni, tarehe 1 Septemba na
tarehe 31 Novemba, 2016 na kuongeza kuwa, Serikali itatoa ushirikiano
mkubwa kwa kampuni hizo kuhakikisha zinatekeleza mipango yao kwa wakati.
Profesa Muhongo alihitimisha
vikao na wawekezaji katika kampuni za utafiti na uchimbaji wa mafuta na
gesi tarehe 24 Februari,2016 ambapo alianza kukutana na wazalishaji
wadogo wa umeme wa chini ya megawati 20 unaotokana na maji mwezi
Janurari, 2016, na wiki ya kuanzia tarehe 15 Februari,2016 alikutana na
wawekezaji mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika sekta ndogo ya
umeme.
No comments:
Post a Comment