Tuesday, 23 February 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Mabalozi wa nchi Tatu

sil2
WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za Uturuki, Ireland na Uswisi pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao leo (Jumanne, Februari 23, 2016), ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwashukuru mabalozi hao kwa kuja kujitambulisha rasmi na kwa pongezi walizokuja kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.

Mapema leo, Waziri Mkuu alikutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez ambaye alimweleza jinsi UNDP imekuwa ikisaidia programu za kukabiliana na
maafa (resilience), ukuaji wa uchumi, utawala bora na masuala ya jinsia.

Alisisitiza haja ya Tanzania kuendeleza kampeni ya kupambana na ujangili na kusisitiza kuwa Umoja huo una nia ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Naye Balozi wa Uturuki, Bibi Yesemin Eralp alimweleza Waziri Mku nia ya nchi kuleta wawekezaji katika nyanja za kilimo, nishati, afya na ujenzi na kusisitiza kuwa kuna haja ya kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwao ili kuimarisha uhusiano uliopo.

“Tunao uwezo wa kifedha na tunao uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia. Tukifungua viwanda hapa nchini, tunaweza kuongeza ajira kwa Watanzania,” alisema.
Naye Balozi wa Ireland nchini, Bibi Fionnuala Gilsenan alimweleza Waziri Mkuu jinsi ambavyo nchi yake imekuwa ikisaidia sekta za kilimo kupitia mpango wa ASDP, bajeti ya Serikali na suala la lishe na urutubishaji wa vyakula (food nutrition and fortification).
“Tulianza na suala la kilimo na bajeti ya Serikali. Hivi sasa tunataka kusaidia kwenye uelimishaji juu ya haki za wanawake, masuala ya uzazi wa mpango, pamoja na kupambana na ndoa za utotoni,” alisema.
“Tumeamua kupigia kelele suala la lishe na urutubishaji wa vyakula kwa sababu lishe duni imechangia kwa kiasi kikubwa udumavu wa watoto wengi. Tulipoanza tatizo hili lilikuwa limeenea kwa asilimia 46 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano lakini sasa limepungua na kufikia asilimia 36 hadi 38,” aliongeza.

Alimuomba Waziri Mkuu Majaliwa alishikie bango suala hilo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kwani mtoto akishadumaa kimakuzi hata akili yake pia inadumaa na tatizo lake haliwezi kurekebishwa kwa tiba yoyote ile.

Naye Balozi wa Uswisi nchini, Bibi Florence Mattli alimweleza Waziri Mkuu nia ya nchi yake kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa miaka 50 ili kukuza viwango vya uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Alimweleza Waziri Mkuu jinsi nchi yake imekuwa ikisaidia kundeleza nyanja za kupambana na rushwa kupitia TAKUKURU na kampeni ya kusaidia kujenga uelewa wa wananchi kupitia vyombo vya habari nchini.

Wananchi waaswa kutunza miundombinu ya barabara inayojengwa kwa ushirikiano na wafadhili

st2
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mhandisi Mussa  Iyombe akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa barabara za Halmashauri nchini unaotekelezwa kwa ushirikiano na shirika la Maendeleo la Japan ( JICA) mradi unaolenga kuwajengea uwezo wahandisi wa Halmashauri na Mikoa katika kusimamia na kukarabati barabara zilizopo katika maeneo yao kwa kushirikiana na wananchi.
st3
Mhandisi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Godwin Mpinzile akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara na ukarabati katika Halmashauri hiyo unaofadhiliwa na JICA ukilenga kuwashirikisha wananchi katika ujenzi na utunzaji wa barabara hizo ili ziweze kudumu
st4
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mhandisi Mussa  Iyombe akimpongeza  Mwakilishi Mkazi wa Shirika la maendeleo la Japan (JICA) hapa nchini bw. Nagase Toshio kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan hali iliyochangia kufanikiwa miradi ya ujenzi wa barabara katika halmashauri mbalimbali hapa nchini inayofadhiliwa na shirika hilo.
st5
Muwakilishi Mkazi wa Shirika la maendeleo la Japan (JICA) bw. Nagase Toshio akifafanua kuhusu ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Japan katika kutekeleza mradi huo unaolenga kujenga uwezo kwa wahandisi wa Halmashauri hapa nchini ili waweze kuwashirikisha wananchi katika miradi ya barabara inayotekelezwa ili waweze kujiletea maendeleo .
st6
Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa  bw. leopold  Runji akitoa ushuhuda wa namna halmashauri hiyo ilivyonufaika na mradi wa ujenzi na ukarabati wa barabara unaotekelezwa katika halmashauri  hiyo kwa ufadhili wa shirika la JICA.

Na Kalonga Kasati

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI bw. Mussa Iyombe amewataka wananchi kutunza barabara zinazojengwa  na Serikali kwa kushirikiana na wafadhili katika Halmashauri zote hapa nchini.

Akizungumza leo Jijini Dar es salaam katika hafla fupi ya kupokea ripoti ya utekelezaji wa mradi wa Ujenzi na ukarabati wa barabara za halmashauri nchini  Iyombi amebainisha kuwa mradi huo umefadhiliwa  na  Shirika  la Maendeleo la Japan (JICA) .
“Mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri  za Iringa,Mufindi,Chamwino na Kondoa” alisisitiza Iyombe.

Akifafanunua kuhusu utekelezaji wa mradi huo  Iyombe amebainisha kuwa  unadhamiria kujenga uwezo kwa wahandisi wa Mikoa na Halmashauri hapa nchini  ili waweze kushirikiana na wananchi katika kujenga  na kulinda miundo mbinu hiyo kwa maslahi ya Taifa.
 Aidha  Iyombi  amewata wakurugenzi wa Halmashauri  ambazo mradi huo unatekelezwa  kutunza barabara hizo ili zilete matokeo yaliyokusudiwa.

Akizungumzia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania Iyombe amesema kuwa maeneo ambayo Tanzania imekuwa ikipata ufadhili kutoka Japan ni Sekta ya Kilimo,Viwanda,Uimarishaji wa Utawala bora.

Kwa upande wake mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) bw. Nagase Toshio amesema kuwa  Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
 
Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa barabara katika Halmashauri hapa nchini unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza imekamilika katika Halmashauri za Chamwino na Iringa na awamu ya pili imekamilika katika Halmashauri za Kondoa na Mufindi ambazo ripoti ya utekelezaji wake iliwasilishwa leo katika mkutano wa siku moja ulifanyika Jijini Dar es salaam ukilenga kufanya tathmini ya utekelezaji kabla ya kuanza kwa awamu ya tatu.

No comments:

Post a Comment