Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim
Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi ya
Waziri Mkuu wakati alipotoa maagizo ya Rais Dk. John Pombe Magufuli
kuhusu mawaziri ambao bado hawajajaza fomu za Tamko
la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha katika
Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam
ifikapo leo saa 12.00 jioni
Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim
Majaliwa akiendelea kufafanua mambo kadhaa kwa wanahabari katika mkutano
huo kushoto ni WAZIRI wa nchi,ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa
Umma na Utawala bora, Mh Angella Kairuki
Na Kalonga Kasati
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema mawaziri ambao hawajajaza
Tamko la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha
katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es
Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni (Ijumaa, Februari 26, 2016).
Agizo hilo la Rais limetolewa leo
na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mbele ya waandishi wa habari katika
mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza
mawaziri ambao hawajajaza tamko la rasilmali au hati ya ahadi ya
uadilifu wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri
ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe
kwenye nafasi yake,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu
amesema wakati akifungua mafunzo ya Mawaziri na Naibu Waziri kuhusu
Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi ya
Uadilifu yaliyofanyika Ikulu jana (Alhamisi, Februari 25, 2016)
alikabidhiwa majina ya Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao hawajawasilisha
Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.
Amewataja
mawaziri wanaotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na
hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw.
Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Bw.
January Makamba. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine
Mahiga ambaye anatakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi
wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce
Ndalichako ambaye anatakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira), Bw. Luhaga Mpina anatakiwa
kurejesha fomu za tamko la rasilmali na madeni pamoja na hati ya ahadi
ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
No comments:
Post a Comment