Na Kalonga Kasati
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Muhongo ametaka kasi iongezwe katika mradi wa ujenzi wa kiwanda
cha uchakataji na usindikaji wa gesi kimiminika unaotarajiwa kuanza
mkoani Lindi mara baada ya taratibu za maandalizi kukamilika.
Profesa Muhongo alisema hayo
katika kikao kwa ajili ya kujadili hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya
ujenzi wa kiwanda hicho kilichoshirikisha watekelezaji wa mradi huo
ambao ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na makampuni
yanayojishughulisha na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi nchini.
Makampuni ya utafiti wa mafuta na
gesi yanayotekeleza mradi huo ni pamoja na Shell, Statoil, Ophir
Energy, Pavilion na Exxon Mobil. Pia kikao hicho kilishirikisha
watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la
Taifa (NDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Wakala wa Jiolojia
Tanzania (GST)
Mara baada ya kupokea taarifa ya
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusindika
gesi kimiminika Profesa Muhongo alilitaka shirika la TPDC kushirikiana
kwa karibu Na makampuni ya utafiti wa mafuta na gesi yanayotekeleza
mradi huo na kwa kasi ya haraka ili mradi huo uweze kukamilika kwa
wakati.
Profesa Muhongo alisema Tanzania
ina utajiri mkubwa wa gesi hivyo ni vyema watekelezaji wakachangamkia
fursa hiyo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusindika gesi
kimiminika ambayo mahitaji yake ni makubwa duniani hususan katika
bara la Asia.
“Ifikapo mwaka 2025 inategemewa
kuwa mahitaji ya gesi duniani yatakuwa ni kiasi cha tani Milioni 440
kwa mwaka hususan katika nchi za Asia ambazo ni karibu na Afrika, hii
ni fursa ambayo tunatakiwa kuichangamkia ili kuendana na soko
itakapofika kipindi hicho,”
alisema Profesa Muhongo.
alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo aliendelea kusema
kuwa gesi ya kimiminika imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa
uchumi wa nchi zinazoendelea huku akitolea mfano wa Algeria ambayo ni
nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na kiwanda cha kuchakata na kusindika
gesi kimimika ambayo kwa sasa imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Katika maandalizi ya awali ya
mradi huo, Profesa Muhongo aliagiza uundwaji wa timu kwa ajili ya Maandalizi ya mradi huo ikishirikisha wataalam kutoka Wizara ya Nishati
na Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Fedha,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), taasisi mbalimbali pamoja
na wawakilishi kutoka katika makampuni yanatofanya utafiti wa gesi na
mafuta nchini ambayo ni mtekelezaji wa mradi huo.
Alisisitiza kuwa ni vyema timu
hiyo ikawa na wataalam wenye uzoefu mkubwa watakaofanya kazi kwa weledi
na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Aliagiza kuwa timu hiyo kukamilisha taratibu zote za maandalizi kabla ya mwezi Novemba, mwaka huu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio
alisema kuwa shirika lake limekuwa likishirikiana na wabia wa ujenzi wa
kiwanda hicho katika hatua zote za maandalizi ya awali na kuahidi
kuongeza kasi ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment