Mkurugenzi Mtendaji kutoka
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee ( wa pili
kutoka kulia) akielezea mikakati ya kampuni hiyo katika uwekezaji wa
uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe mbele ya Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na Watendaji kutoka Wizara
ya Nishati na Madini na Taasisi zake.
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo ( kulia) akimweleza Mkurugenzi Mtendaji kutoka
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee (kushoto)
fursa za uwekezaji nchini kwenye sekta ya umeme.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo katika kikao hicho
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee akifafanua jambo katika kikao hicho.
Na Kalonga Kasati
Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka taasisi zinazosimamia miradi
ya umeme nchini kuongeza kasi ya utendaji kazi ili Tanzania iweze
kupata umeme wa uhakika.
Profesa Muhongo aliyasema hayo
katika kikao chake kilichokutanisha Kampuni ya Uchimbaji Madini ya
Kibo Mining na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema kuwa ili nchi iweze kuwa
na umeme wa uhakika unaozalishwa kwa wakati ni lazima taasisi
zilizopo chini ya Wizara zikahakikisha zinaongeza kasi katika uwekezaji
kwenye Uzalishaji wa umeme kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani na
nje ya nchi wenye vigezo ili uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi na
kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ambayo
ni kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika kundi la nchi masikini
Duniani
na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka
2025.
Alisisitiza kuwa ili kufikia
lengo hilo ni lazima taasisi zikaongeza kasi katika miradi yake ya Umeme, kwa kushirikiana na wawekezaji mbalimbali na kuwataka kuondoa
urasimu kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye miradi ya
uzalishaji wa umeme nchini.
Aliongeza kuwa nishati ni roho ya
uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa hakuna nchi yoyote Duniani iliyopiga
hatua bila kuwa na nishati ya umeme ya uhakika.
“ Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inakua kwa kasi na kutoa
ajira hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo nishati ya umeme
inahitajika sana; bila nishati ya uhakika uchumi hauwezi kukua kwa
kasi inayotakiwa,’ alisisitiza Profesa Muhongo.
Waziri Muhongo aliendelea kusema
kuwa nishati ya umeme ya uhakika itachangia ukuaji wa sekta za
viwanda vidogo hasa maeneo ya vijijini, kilimo kukua kwa kasi na
hivyo kunufaisha wananchi na pato la taifa kukua kwa kasi.
Aidha Profesa Muhongo alilitaka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji (EWURA) kushirikiana kwa pamoja katika hatua zote za
uwekezaji nchini ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kujitokeza kati ya
serikali na wawekezaji.
“TANESCO na EWURA naomba
mshirikiane katika kila hatua, kwa kukaa meza moja na wawekezaji na
kufikia mwafaka kabla hawajaanza kuwekeza”, alisema Profesa Muhongo
Awali Mkurugenzi Mtendaji kutoka
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee akizungumza
katika kikao hicho, alisema kuwa kampuni ya Kibo Mining ina mpango wa
kuwekeza katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe ambapo
itaanza na Ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya
mawe wa Megawati 900 kwa awamu tofauti.
Alisema awamu ya kwanza ambayo ni Ujenzi wa mtambo wa kuzalisha Megawati 300 utakaogharimu Dola za
Marekani milioni 800 utakamilika ifikapo mwaka 2019.
Akielezea hatua iliyofikia ya
maandalizi ya uwekezaji wa kampuni ya Kibo Mining Coetzee alisema kuwa
kampuni hiyo iliyoanza maandalizi yake mwaka 2008 inakamilisha
upembuzi yakinifu (feasibility study) katika mradi wake na kuongeza
kuwa wana mpango wa kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza mwaka 2017 baada
ya taratibu zote kukamilika
.
Alisema mara Baada ya ujenzi wa
mtambo wa kwanza kukamilika mwaka 2019, umeme Utakaozalishwa mbali na
kutumika viwandani utaongezwa kwenye gridi ya taifa na hivyo
kupunguza changamoto ya ukosefu wa umeme nchini.
No comments:
Post a Comment