SERIKALI KUTOA MIKATABA MAALUM YA AJIRA SEKTA YA UJENZI
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro Bw. Amos Makala walipokutana mjini Moshi kwa ziara ya
ukaguzi wa miradi iliyo chini ya sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika kampuni ya Dott Services Limited inayojenga barabara ya Same-Mkumbara Km 96. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
wafanyakazi wa kampuni ya Dott Services Limited wakishangilia
kwa furaha baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa kumtaka mkandarasi kuwalipa madai yao yote ifikapo
Februari 26, mwaka huu.
Muoneano wa Jengo la Kituo cha Forodha cha pamoja (One Stop Border Post) kwa upande wa Tanzania lililopo Holili.
Ujumbe wa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ukielekea katika kituo cha
pamoja cha forodha (One Stop Border Post) kwa upande wa Taveta nchini
Kenya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata ufafanuzi wa namna ya kituo cha
pamoja cha Forodha kinavyofanya kazi kutoka kwa Meneja Forodha kwa
upande wa Taveta – Kenya Bw. Daniel Nyambaka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiagana na Meneja Forodha kwa upande
wa Taveta – Kenya Bw. Daniel Nyambaka mara baada ya kukagua kituo hicho.
Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema iko mbioni
kukamilisha mkataba maalumu wa ajira utakaotumiwa na makandarasi wote
nchini katika kuajiri watanzania wazalendo kwenye miradi ya ujenzi
inayosimamiwa na sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa
barabara ya Mkumbara-Same yenye urefu wa Km 96 mkoani Kilimanjaro.
Amemtaka mkandarasi Dott Services Limited kukamilisha hatua za mwisho za ujenzi wa barabara hiyo na kulipa stahili zote za wafanyakazi kwa mujibu wa mikataba.
“Nakupa mwezi mmoja kukamilisha
ujenzi uliobaki wa barabara hii pia hakikisha kila mfanyakazi ambaye
amemaliza mkataba wake analipwa stahili zake zote kwa muda usiozidi siku
mbili”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemuagiza Mkuu wa
Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi kufatilia kwa makini madai ya
wafanyakazi wazalendo ya malipo ya likizo, mafao ya NSSF, malimbikizo ya
mishahara, matibabu na mazingira magumu ya kazi ili yalipwe sambasamba
na madai mengine na hivyo kuondoa malalakimiko yaliyopo na yanayoweza
kujitokeza mara baada ya kukamilika kwa mradi.
“Kuanzia sasa mameneja wa
TANROADS wahakikishe kwenye ujenzi wa barabara na miradi iliyo chini ya
wizara hii kazi ambazo watanzania wanaweza kuzifanya zisifanywe na
wageni kwani hali hiyo huwanyima haki watanzania wenye ujuzi wa kuijenga
nchi yao”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara
Nchini (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro Eng. Marwa Rubirya amemhakikishia
Waziri Mbarawa kuwa kwa sasa km 1,020 za mtandao wa barabara wilayani
Same zinapitika na serikali imeanza kuongeza kiwango cha barabara za
lami Wilayani humo ikiwemo ujenzi wa barabara ya
Same-Kisiwani-Maore-Ndungu na Kihuriyo hadi Mkomazi.
Amemhakikishia Waziri Prof.
Mbarawa kwamba TANROADS itaendelea kuhakikisha barabara za milimani
wilayani Same ambazo ni sawa na asilimia 75 ya barabara zote wilayani
humo zinapitika wakati wote wa mwaka kutokana na umuhimu wake kwa
shughuli za kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same Bw.
Herman Kapufi amemuomba Waziri Mbarawa kuzipandisha hadhi barabara za
Hedaru-Vunta-Miamba Km 41.2, Bangarara-Chome-Ikokoa Km 25.6, na
Ndungu-Lugulu Km 8 ili zihudumiwe na TANROADS kutokana na umuhimu wake
kiuchumi na kijiografia.
Katika hatua nyingine Waziri
Mbarawa amekagua kituo cha pamoja cha forodha kilichopo Holili
(Tanzania) na Taveta (Kenya) na kuona shughuli za usafirishaji na
uchukuzi zinavyoendeshwa na kusisitiza umuhimu wa kituo hicho
kufanyakazi kwa kushirikiana ili kuongeza mapato kwa nchi za Kenya na
Tanzania.
No comments:
Post a Comment