Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kuhusu ukusanyaji
madeni ambayo Wakala wa Majengo nchini (TBA) inadai wapangaji wake.
Muonekano wa barabara ya
Sakina-Tengeru Km 14.1 inayojengwa kwa njia nne kwa kiwango cha lami ili
kupunguza msongamano wa magari kuingia na kutoka katikati ya jiji la
Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi M/S
Hanil Jiangsu J/V anayejenga barabara ya Sakina-Tengeru Km 14.1 na
barabara ya mchepuo wa kusini Arusha bypass Km 42.4 jijini Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia) akikagua ripoti ya biashara
inayofanywa na Kampuni ya Simu nchini (TTCL), jijini Arusha. Wa tatu
kulia ni Meneja Kanda ya Kaskazini TTCL Bw. Peter Lusama.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) akiimba wimbo wa mshikamano
daima na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini
TANROADS kabla ya kufungua rasmi mkutano wa sita wa Baraza hilo. Kulia
ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale na kushoto ni Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza kufanya kazi kwa malengo
yanayopimika katika kikao chake na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini
ya wizara yake, jijini Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisikiliza maelezo ya namna ya
kuhamisha miundombinu ya maji pembeni ya Barabara ya Sakina-Tengeru
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa Makandarasi wote
nchini kuhakikisha wanasaini mikataba ya ajira na wafanyakazi katika
miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote.
Akizungumza jijini Arusha mara
baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya
Sakina-Tengeru yenye urefu wa Km 14.1 na barabara ya mchepuo ya kusini
(Arusha bypass) yenye urefu wa Km 42.4, Prof. Mbarawa amesema mkandarasi
atakayeshindwa kutoa mikataba kwa mujibu wa sheria za Tanzania,
atanyang’anywa kazi ya ujenzi kwa kuvunja sheria.
“Barabara zinajengwa kwa kodi za
wananchi hivyo wajenzi wa barabara nao ni lazima wafuate sheria za nchi
ili kuhakikisha Serikali inapata kodi stahili na wafanyakazi wazawa nao
wanapata haki stahili kwa mujibu wa ajira zao”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Amezitaka taasisi za TRA, NSSF na
nyingine zinazosimamia ajira za wafanyakazi kufuatilia miradi ya ujenzi
ili kuona fursa za mapato ambazo serikali inaweza kupata na kusajili
wafanyakazi katika hifadhi ya mifuko ya jamii.
Waziri Prof. Mbarawa amewataka
mameneja wa tanroads na maafisa kazi kukagua mikataba ya Ajira za ujenzi
katika maeneo yao ili kuona haki inatendeka kwa makandarasi na kwa Wafanyakazi ili ujenzi wa barabara ukamilika kwa wakati na kwa ubora
unaotakiwa.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amefungua mkutano wa Sita wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS) na kuwataka kuweka mikakati itakayowezesha
kulinda hifadhi ya barabara, kudhibiti magari yanayozidisha uzito na
kusimamia kasi katika miradi ya ujenzi wa barabara.
“Mmekua mkifanya kazi nzuri,
endeleeni kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi, weledi na kujiwekea Malengo
ya kujipima mwaka hadi mwaka ili muendelee kuwa tassisi ambayo watu
watakuja kujifunza kwenu”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS
Eng. Patrick Mfugale amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa TANROADS
imejipanga kuhakikisha miradi ipatayo 90 ya ujenzi wa barabara
inayoendelea nchini kote inakamilika katika ubora unaotakiwa na unao
uwiana na thamani ya fedha.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa
amemuagiza Meneja wa Wakala wa Majengo nchini (TBA), mkoa Wa Arusha, Bw.
Victor Baltazar kukusanya madeni yote kwa haraka ili kukamilisha miradi
ya Ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na za biashara inayosimamiwa na
Wakala huo mjini Arusha kukamilika kwa wakati.
Prof. Mbarawa ambaye yuko katika
ziara ya mikoa ya kanda ya kaskazini amezitaka taasisi zilizo chini wa
wizara hiyo kuhakikisha zinafanya kazi kibiashara ili kuboresha mapato
ya Serikali na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NEC NA UNDP ZAFANYA MIKUTANO YA MAJADILIANO KUBORESHA UTOAJI ELIMU YA MPIGA KURA
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi
Bw. Ramadhan Kailima alipozindua kituo Cham mawasiliano ambapo Jumla ya
Simu 1,381 zilipokelewa katika kituo cha Mawasiliano cha Tume ya Taifa
ya Uchaguzi – Nec Call Center, kilichoanzishwa mahususi kwa lengo la
kuwasaidia wapiga kura pamoja na wadau mbalimbali wa uchaguzi ili kupata
elimu ya mpiga kura.
Na Mwandishi Wetu
Hivi karibuni, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwa kushirikiana na Mradi wa ukuzaji wa Demokrasia nchini (DEP)
chini ya shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) iliandaa mikutano ya
tathmini ya utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka
jana ili kujadiliana juu ya kuboresha utoaji wa Elimu hiyo katika
Chaguzi na kuboresha ushirikiano kati ya Tume na Wadau mbalimbali wa
Uchaguzi.
Mikutano hiyo pia ililenga
kuainisha maeneo ambayo wadau wanataka yafanyiwe marekebisho ili
kuboresha utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kukuza
Demokrasia nchini na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati
wa Chaguzi.
Mikutano hiyo ilifanyika kwa
Kanda kwa kuwashirikisha Mwenyekiti wa Tume na Makamishna, Mkurugenzi wa
Uchaguzi Wakuu wa Idara pamoja na Maafisa Kutoka Tume ya Taifa ya
uchaguzi na Mikoa iliyoalikwa kwenye Mkutano huo.
Mikutano hii ilifanyika kuanzia
Februari 2 hadi 11, mwaka huu katika miji ya Manyara, Arusha,
Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya, Rukwa na Katavi. Miji mingine
ni pamoja na Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Unguja, Pemba, Dodoma,
Singida, Tabora, Kigoma, Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu,
Ruvuma, Njombe na Iringa.
Aidha, Mikutano hiyo
ilishirikisha wadau mbalimbali wa Uchaguzi wakiwemo wawakilishi wa Asasi
za Kiraia wa makundi mbalimbali ya jamii kama vile Wanawake, Vijana,
Watu wenye Ulemavu, na Wazee. Wengine ni Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa
(Regional Election Coordinators), Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo
ambao pia ni Wakurugenzi wa halmashauri (Rertuning Officers), Maafisa
Uchaguzi na Maafisa Habari kutoka kila Halmashauri ulipofanyika mkutano
wa wadau.
Kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha
4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, imepewa jukumu la kutoa Elimu ya Mpiga Kura na kusimamia
Asasi, Makundi au watu wanaotoa Elimu hiyo.
Kwa kuzingatia umuhimu wa jukumu
hilo, Tume ilishirikisha Asasi za Kiraia 447 katika kuhamasisha wananchi
na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kushiriki na kujitokeza kujiandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na pia kushiriki katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Asasi za Kiraia ni wadau wakubwa
katika mchakato wa Uchaguzi kwa kuzingatia ukweli kwamba Tume ya Taifa
ya Uchaguzi peke yake haiwezi kuwafikia Watanzania wote kutokana na
kutokuwa na rasilimali watu ya kutosha katika kuwafikishia Elimu ya
Mpiga Kura pamoja na utaalamu mbalimbali wa utoaji wa Elimu hasa jinsi
ya kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu, wanawake, vijana
pamoja na wale walioko pembezoni na maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa
sababu mbalimbali zikiwemo za miundombinu
No comments:
Post a Comment