Thursday 27 July 2017

Wataalam Wakutana Kujadili Upatikanaji Maji kwa Asilimia Mia Ifikapo 2030

1Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa wadau wa maji kutoka nchi 25 za Bara la Afrika wa kujadili kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia mia moja ifikapo mwaka 2030. Mkutano huo umefunguliwa jana Jijini Dar es Salaam.
2Katibu Mtendaji wa Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika (AMCOW), Dkt. Conisius Kanangire akielezea malengo ya mkutano wa wadau wa maji kutoka nchi 25 za Bara la Afrika wa kujadili kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia mia moja ifikapo mwaka 2030. Mkutano huo umefunguliwa jana Jijini Dar es Salaam.
3Wadau wa maji kutoka nchi 25 za Bara la Afrika wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge (hayupo pichani) iliyohusu majadiliano kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia mia moja ifikapo mwaka 2030. Mkutano huo umefunguliwa jana Jijini Dar es Salaam.
4Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa maji kutoka nchi 25 za Bara la Afrika waliokutana Jijini Dar es Salaam kujadili kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia mia moja ifikapo mwaka 2030.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wataalam wa masuala ya maji kutoka nchi 25 za Bara la Afrika wamekutana kujadili njia zitakazowezesha upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini ifikapo mwaka 2030.
Mkutano huo umefunguliwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ambaye amesema kuwa  majadiliano hayo yameanzishwa baada ya azimio la Umoja wa Mataifa Namba 6 kuzitaka nchi zote Duniani kuhakikisha kuwa wananchi wao wanapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka huo.
“Ili kuhakikisha agizo la Umoja wa Mataifa linatekelezwa, nchi za Umoja wa Afrika ziliamua kuunda kamati za wataalam watakaojikita katika kupanga mikakati endelevu ya kutekeleza agizo hili,”alisema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi Lwenge ameongeza kuwa baada ya majadiliano hayo wataalam watapeleka taarifa katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika (AMCOW) kinachotegemewa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu ili kuweza kupata tathmini ya kila nchi namna inavyotekeleza azimio hilo.
Aidha, Mhandisi Lwenge amefafanua kuwa kwa miaka mitano ijayo, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanaokaa mijini wanapata maji safi na salama kwa asilimia 95 na vijijini asilimia 85, uondoaji wa maji taka kwa asilimia 30 pamoja na kuhakikisha nyumba za vijijini zina vyoo.
 
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa AMCOW, Dkt. Conisius Kanangire amesema kuwa mkutano huo umewashirikisha wataalam pamoja na wadau kutoka mashirika mbalimbali yanayohusika na uangalizi wa mabonde ya maziwa na mito Afrika ili nao waweze kutoa mchango wa mawazo utakaopelekea nchi za Afrika kuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya maji.  
”Baraza la Mawaziri wa Maji pekee haliwezi kuleta mafanikio makubwa tunayoyataka kwa Afrika ndio maana tumeamua kuwashirikisha wataalam wa maji kutusaidia namna ambavyo tutaweza kuwa na mikakati mizuri ambayo itawezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa nchi zote,” alisema Dkt. Kanangire.
Dkt. Kanangire ameishkuru Serikali ya Tanzania kwa kushiriki bega kwa bega katika kuhakikisha baraza hilo linafanya kazi nzuri hivyo anategemea kuwa kikao hicho kinachoendelea nchini kitatoa majibu ya uhakika juu ya upatikanaji wa maji safi na salama.   

No comments:

Post a Comment