Thursday 27 July 2017

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Albert Msole (CCM) ashinda tena

IMG_20170721_152504
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Albert Msole akiomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kushikilia nafasi hiyo kwenye baraza la madiwani ambapo alichaguwa tena kwa mwaka 2017/2018 na madiwani hao 
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Albert Msole (CCM) amefanikiwa kushinda tena nafasi hiyo baada ya kumbwaga mpinzani wake Philemon Oyogo (Chadema).    
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi akitoa matokeo hayo alisema kati ya madiwani 22 waliopiga kura, madiwani 14 walimpigia Msole na madiwani nane walimpigia Oyogo. 
Myenzi alisema Msole atadumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2017/2018 ndipo utakapofanyika uchaguzi mwingine wa makamu Mwenyekiti. 
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo Msole aliwashukuru madiwani wote kwa heshima kubwa waliyompa na kumrudishia tena nafasi hiyo hivyo ataendelea kushirikiana nao kuhakikisha kuwa halmashauri hiyo inasonga mbele kwenye maendeleo. 
“Tuendelee kushirikiana pamoja kwani tumeshirikiana vizuri tangu mwaka 2015 na kazi yangu kubwa ni kumsaidia Mwenyekiti wa halmashauri yetu, natoa ahadi kwenu kuwa nitaendelea kuteleleza wajibu wangu kwani heshima mliyonipa ni kubwa japo mimi ni mdogo kwenu,” alisema Msole.  
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jackson Sipitieck alisema kama siyo jambo la kisheria, kanuni na taratibu, wasingeruhusu uchaguzi huo ufanyike kwani jitihada za Msole za uchapakazi kwenye halmashauri hiyo zinajulikana. 
 
“Msole ni mpambanaji mzuri, muwajibikaji, muwazi na anayefanya kazi zake kwa kutenda haki bila kupendelea mtu na nadhani wote tunatambua jitihada zake kama siyo sheria angekuwa makamu Mwenyekiti kwa miaka yote mitano,” alisema Sipitieck.
Alitangaza wajumbe wa kamati ya fedha, uongozi na mipango ni Alamayan Ranga na Grace Mtataiko, Mwenyekiti wa kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira, Loishiye Lesakwi  na Mwenyekiti wa kamati ya jamii, Sendeu Laizer. 
Aliwataja wajumbe wa kamati ya maendeleo ya jamii ni Julius Mamasita, Ngaidiko Tipai, Philemon Oyogo, Haiyo Mamasita, Michael Haiyo, Nyika Shawishi na Ezekiel Lesenga Mardadi. 
Alisema wajumbe wa kamati ya uchumi ni Lucas Moringe, Christopher Kuya, Saimon Kikoda, Naishorwa Tunay, Paulina Makeseni, Rehema Namani, Thomas Yohana na Diana Kuluo.

No comments:

Post a Comment