Friday 21 July 2017

Taarifa kuhusu Madini


nembo 3_thumb[1]
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kuutarifu umma kuwa, kufuatia kupitishwa kwa Sheria Mpya ijulikanayo kama The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2017 iliyoanza kutumika tarehe 7/7/2017, kumefanyika Marekebisho kadhaa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.
Marekebisho makubwa yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ni pamoja na;
  • Kuanzishwa kwa Tume ya Madini (Mining Commision);
  • Kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (Tanzania Mineral Audit Agency- TMAA);
  • Kuongezeka kwa malipo ya Mrabaha kutoka asilimi 4 (4%) kwa madini ya Metali (mfano dhahabu, shaba, fedha n.k) hadi asilimia 6 (6%);
  • Kuongezeka kwa malipo ya Mrabaha kutoka asilimia 5 (5%) kwa madini ya almasi na vito (mfano Tanzanite, Ruby, Garnets n.k) hadi asilimia 6 (6%).
Aidha, kupitia Marekebisho ya Sheria ya Fedha na Sheria ya Kodi, hivi sasa kila Mtu au Kampuni anayetaka kusafirisha madini nje yatakaguliwa na kuthaminishwa na atalipa ada ya ukaguzi (clearing fees) ambayo ni asilimia 1 (1%) ya thamani ya madini anayosafirisha.
Pia, Mchimbaji mdogo anayeuza madini kwa Broker au kwa Dealer atakatwa asilimia 5 (5%) ya thamani ya madini kama Withholding tax ambayo itakusanywa na Broker au Dealer na kupelekwa TRA. Pamoja na kufutwa kwa TMAA na Ofisi za Madini za Kanda, watumishi waliokuwa wanafanya kazi kwenye Taasisi/Ofisi hizo ambao hawana tuhuma zozote wanaendelea na ajira zao kwa sababu ni Watumishi wa Serikali katika Wizara ya Nishati na Madini. Hivyo, watumishi hao watatumika katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Wizara ya Nishati na Madini ikiwa ni pamoja na;
  • Kukusanya maduhuli ya Serikali yanayotokana na madini ya Ujenzi na madini ya viwandani na pia kuhakiki Vocha za malipo ya mrabaha;
  • Kukagua migodi ya Wachimbaji Wakubwa, Wachimbaji wa Kati na Wachimbaji wadogo;
  • Kukagua miradi yote ya wazalishaji dhahabu kutokana na marudio kupitia teknolojia ya Vat leaching;
  • Kukagua maeneo ya Viwanja vya ndege, bandari na mipakani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini;
  • Kupokea malipo ya tozo mbalimbali kwa mujibu wa Sheria ya Madini na kutoa huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo; na
  • Kusimamia masuala yote ya usalama migodini.
  •  
Katika kipindi hiki cha mpito kabla Tume ya Madini haijaundwa, shughuli hizi zote zitafanyika chini ya usimamizi wa Kamishna wa Madini.
Aidha, katika kipindi hiki cha mpito, Serikali imesimamisha utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji madini hadi hapo Tume ya Madini itakakapokuwa imeundwa na kuanza kazi rasmi.
Hivyo, Wizara inawasisitiza wadau na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano kwa Watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini kama ambavyo mmekuwa mnafanya siku zote kusudi kuwe na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini hususan katika masuala ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika kipindi hiki cha mpito.
Imetolewa na;
Prof. James E. Mdoe
KAIMU KATIBU MKUU
21 Julai, 2017

No comments:

Post a Comment