Monday 31 July 2017

Waziri Mkuu Majaliwa:Waharibifu vyanzo vya maji kukiona cha moto

Waziri Mkuu amewataka watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
Waziri Mkuu amesema wananchi lazima wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
"Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria", amesema Majaliwa.
Mbali na hayo Mh. Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya iliyotengewa sh. bilioni 2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.
Amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, Majaliwa amesema mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383  kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 2.72 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wilaya ya Rungwe.

No comments:

Post a Comment