Sunday, 14 February 2016

mu3
Penny mara baada ya kushinda medali katika mashindano ya Olimpiki

Muogelaji nyota wa zamani wa dunia na mshindi wa medali ya dhahabu ya michezo ya Olimpiki kwa upande wa kike, Penelope “Penny” Heyns wa Afrika Kusini ataendesha mafunzo ya siku mbili ya kuogelea  kwa makocha wa klabu maarufu ya mchezo huo hapa nchini,  Dar Swim Club.
Penny ambaye ni bingwa wa kihistoria wa michezo ya Olimpiki kwa staili ya ‘Breastroke’ atawasili nchini Alhamis akitokea nchini Afrika Kusini tayari kuendesha  mafunzo hayo kwa makocha watano wa klabu hiyo.

Katibu Mkuu wa Dar Swim Club, Inviolata Itatiro alisema jana kuwa maandalizi yamekamilika na klabu yao itagharimia mafunzo hayo kwa lengo la kuboresha viwango vya wachezaji wao na makocha kwa ujumla.

Inviolata alisema kuwa makocha wao watakaoshiriki katika kozi hiyo kuwa ni Michael Livingstone, Ferick Kalengela, Radhia Gereza, Kanisi Mabena, Adam Kitururu, Simon Ngoya na Salum Mapunda.

Alisema kuwa makocha wao wanasifa za ngazi ya juu ya ufundishaji wa mchezo huo, kutokana na kukua kwa kasi kwa mchezo huo, wameona bora wapate mbinu za kisasa ili kwenda na wakati.
“Makocha wetu wote watano ni bora katika ufundishaji, waliwahi kupata mafunzo Dubai,  Marekani na nchi mbalimbali, lakini klabu imeona kuendelea kuwapa mbinu zaidi ili kufikia malengo yetu ya miaka 10,”
“Tunataka kuona kila mtoto anacheza mchezo wa kuogelea, tulianza na watoto wadogo ambao kwa sasa ni mastaa katika mchezo huo na kuweza kushinda medali mbalimbali nje ya nchi,” alisema Inviolata.
Alisema kuwa wao wameamua kupromoti mchezo wa kuogelea kwa vitendo ili kuona siku moja watanzania wanafuzu kushindana michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya madola na mashindano ya dunia siyo kupata nafasi za upendeleo kama ilivyo sasa.
Alifafanua kuwa Penny alitwaa medali za dhahabu katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Atlanta 1996 kwa mita 100 na 200 na wanaamini kuwa ujio wake utapandisha morali wachezaji wao na makocha.
Wakati huo huo;  klabu hiyo imeendesha zoezi la ukusanyaji fedha kwa ajili ya kufanikisha semina hiyo na kufikia lengo lake.
Inviolata alisema kuwa zoezi hilo limefanikiwa kutokana na msaada wa wadhamini mbalimbali ambao ni Best Western (Coral Beach Hotel), Euopcar, Butcher Shop Dar es Salaam, CapeTown Fish Market, Warere, Lemon Spa,Pyramid Consumers, Instyle Hair and beauty salon, Coca Cola, Zen Spa, Karambezi Cafe, The Water Front na Southern Sun Dar es Salaam.
“Nawapongeza watu waliochangia na kufanikisha zoezi hili, makocha na waogeaji wetu watapata mafunzo bure na si kwa kuwabana wazazi au walezi wao kama ilivyokuwa awali,” alisema Inviolata.

SHEREHE ZA KANISA WAADVENTISTA WASABATO MTAA WA MANZESE ZAFANA

in1
Jeshi la vijana Watafuta Njia (PFC) wakionesha programu maalum katika sherehe ya kumuaga Mch. Amosi Lutebekela (hayupo pichani) iliyofanyika katika kanisa la waadventista wasabato Manzese jana.
in2
Kwaya ya wasabato ya Mbiu wakikabidhi zawadi ya kwaya kwa Mch. Amosi Lutebekela na Mkewe kwenye sherehe ya kuwaaga iliyofanyika jana katika kanisa la wasabato Manzese.
in3
Kwaya ya Wasabato Ruvu kitonga wakimtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji wakati wa sherehe ya kumuaga Mch. Amosi Lutebekela iliyoandaliwa na kanisa la wasabato mtaa wa Manzese.
in4
  Kwaya ya Angaza wakiimba wimbo maalum wa kumuaga Mch. Amosi Lutebekela kwenye sherehe ya kumuaga iliyoandaliwa na kanisa la wasabato mtaa wa Manzese.

Na. Kalonga Kasati
Mkurugenzi wa Sauti ya Unabii, Uchapaji na Maeneo Mapya Mch. Amosi Lutebekela jana amekemea tabia mbaya ya baadhi ya waumini wa kanisa la waadventista wasabato wanaoshindwa kutimiza kiapo chao cha ndoa na kuanza kudai kuvunja ndoa kwa sababu zisizokubalika kibiblia.
Akizungumza wakati wa ibada kuu katika kanisa la waadventista wasabato Manzese, jijini Dar es Salaam, Mch. Lutebekela alisema hivi karibuni idadi ya wanandoa ambao wanaomba kuvunja ndoa inaongezeka tena kwa sababu zisizokubalika kibiblia.

“Mimi kama msajili wa ndoa nimekuwa nikishughulikia  changamoto mbalimbali za wanandoa ambao wamekuwa wakiomba kuvunja ndoa kama suluhisho la migogoro yao. Ninakemea wanandoa wote wenye malengo ya kuvunja ndoa kinyume na utaratibu wa biblia. Tabia hiyo ikome mara moja kwa jina la Yesu, alisisitiza.

Katika hotuba yake vilevile Mch. Lutebekela aliwataka vijana ambao hawajaingia katika ndoa kuzingatia sifa za kiroho zaidi badala ya kutegemea mivuto ya kimwili yaani sura nzuri na muonekano wa nje. “Ninapenda kuwaasa vijana wa kiume na wakike epukeni sana kutafuta wenzi wa maisha kwa kuangalia mivuto ya nje yaani sura na muonekano. Sura inachakaa lakini roho na tabia njema haitachakaa hata umri wenu ukisonga, alifafanua Mch. Lutebekela.

Mch. Amosi Lutebekela aliyasema hayo katika sherehe ya kumuaga rasmi iliyoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa wa Manzese baada ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa Sauti ya Unabii, Uchapaji na Injili katika maeneo mapya hivi karibuni. Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi, Mch. Lutebekela alikuwa mchungaji anayesimamia Mtaa wa Manzese.

No comments:

Post a Comment