Monday 28 August 2017

Wenger awataka mashabiki kudumisha imani

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amewaomba mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuwa na imani baada ya kile alichosema kuwa ni uchezaji wa kusikitisha sana baada ya klabu hiyo kucharazwa na Liverpool 4-0 katika mechi ya Ligi ya Premia Jumapili.
Gunners hawakuwa na kombora hata moja lililolenga goli baada ya uchezaji mbaya ambao ulikosolewa pakubwa na mashabiki na wachanganuzi wa masuala ya soka.
"Iwapo baadhi ya watu wanahisi kwamba mimi ndiye tatizo, basi naomba radhi kwamba mimi ndiye tatizo," Wenger aliambia Sky Sports.
"Lakini tunataka mashabiki wetu waendelee kuwa nasi hata baada ya uchezaji mbaya hivyo na kushindwa."
Aliongeza: "Jambo pekee ambalo tunaweza kufanya ni kurejea na kucheza vyema."
Wenger alitia saini mkataba wa miaka miwili mwishoni mwa msimu uliopita, licha ya baadhi ya mashabiki kumtaka aondoke.
Klabu hiyo ilimaliza nafasi ya tano ligini msimu uliopita na kumaliza nje ya nafasi za kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 21 ambayo wamekuwa na Wenger.
Wenger alimwacha mchezaji aliyenunuliwa pesa nyingine na klabu hiyo Alexandre Lacazette kwenye benchi wakati wa mechi hiyo Anfield, lakini alimchezesha Alexis Sanchez kwenye kikosi cha kuanza mechi mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu.
Hata hivyo, vijana wake walipanguliwa na mabao kutoka kwa Roberto Firmino, Sadio Mane, Mohamed Salah na Daniel Sturridge.
Alipoulizwa nini kilikuwa kibaya na uchezaji wa vijana wake, Wenger alisema "kila kitu".
Arsene Wenger ambaye ameongoza Arsenal tangu 1996 alitia saini mkataba wa miaka miwili Mei
"Hatukuwa katika kiwango kifaacho tangu dakika ya kwanza - kimwili, kiufundi na kiakili - na tuliadhibiwa," alisema Mfaransa huyo.
"Uchezaji wetu leo haukubaliki. Ni kweli kwamba leo tulikuwa wapinzani wepesi kwa Liverpool.



Wenger: Marefa wanalindwa kama simba
"Uchezaji wetu ulikuwa mbaya mno. Sitaki kutekwa na hisia, lakini tuna safari ndefu, na kuna sababu zinazosababisha hilo, na wachezaji sasa wanaelekea kwenye mapumziko ya mechi za kimataifa, lakini lazima tujifunze kutokana na uchezaji wetu leo."

No comments:

Post a Comment