Friday 25 August 2017

Meya Jacob:Bomoa bomoa imekuwa kisiasa zaidi

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amefunguka na kudai suala la bomoa bomoa kwa watu waishio maeneo ya Jiji la Dar es Salaam limekuwa la kisiasa zaidi na kuhusisha chama kimoja pekee.
Meya Jacob ameeleza hayo baada ya wakazi waliobomolewa nyumba zao kupaza sauti katika vyombo mbalimbali vya habari ambapo baadhi yao wakidai walichofanyiwa haikuwa sawa kwa kuwa ni miaka mingi wamekuwa wakiishi katika hayo maeneo.
"Bomoa bomoa imeathiri sana watu wa Ubungo, hili linaendeshwa kisiasa zaidi na limekuwa ni la chama kimoja, hatupewi nafasi sisi ya kusikilizwa kwa maana ukiangalia sehemu zingine zilizofanywa miradi kama hii waliitwa na kukaa mezani wakapewa 'compassion' zao, wakalipwa. Nasema ni la chama kimoja kwa sababu haiwezekani kama kuna amani ukaja kuvunja na mapolisi", alisema Jacob.
Pamoja na hayo, Meya Jacob ameendelea kusema "hatma ya watu wanaolia na waliofariki kutokana na bomoa bomoa anayo Mhe. Rais Magufuli kwani yeye ndiyo anaweza akasababisha watu wazidi kuumia na kufa na yeye pia ndiyo mwenye uwezo wa kuwafuta machozi watu hao wakawa na furaha".

Kwa upande mwingine, Meya Jacob ameuomba Rais Magufuli aliangalie suala la bomoa bomoa kwa wakazi wa Manispaa ya Ubungo kwa jicho la ukaribu.

No comments:

Post a Comment