Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Profesa James Mdoe akihutubia wajumbe wa Baraza la
Uongozi wa Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC) jijini Dar
es Salaam baada ya Kituo hicho kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa
kwake.
Mwakilishi Mkazi wa Masuala ya
Uchumi kutoka Ubalozi wa China, Lin Zhiyong mmoja wa wafadhili wa AMGC
akikabidhi zawadi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo, Ibrahim Shaddad kwa
ushirikiano mwema uliopo kati yao.
Balozi wa Msumbiji Nchini
Tanzania, Monica Patricio Clemente akichangia hoja katika Mkutano wa
Baraza la Uongozi wa AMGC jijini Dar es salaam.
Wajumbe mbalimbali wa Mkutano wa Baraza la Uongozi wa AMGC wakiwa katika kikao cha 37 nchini Tanzania.
Jonas kamaleki- MAELEZO
Tanzania imechaguliwa kwa mara ya
pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Madini
na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC).
Uchaguzi huo umefanyika leo jijini
Dar es Salaam katika Mkutano wa 37 wa Baraza hilo uliofunguliwa jana na
Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Wajumbe wa Mkutano huo ambao ni
mawaziri wa wanaohusika na sekta ya Madini wameipitisha Tanzania kwa
kauli moja kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo kutokana na juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John
Pombe Magufuli wa kudhibiti na kusimamia raslimali Madini pia mabadiliko
yanayofanywa kituoni hapo.
Akizungumza kwa niaba ya
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la AMGC, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Prof. James Mdoe amesema Tanzania inathamini mchango
wa Kituo hicho na kuongeza kuwa ndio maana Waziri Mkuu alifungua Mkutano
wa Baraza.
Prof. Mdoe amewakumbusha nchi
wanachama umuhimu wa kutumia Kituo hicho kwani kina vifaa vya kisasa vya
kufanya uchunguzi wa maji na Madini ya kila aina.
Aidha, Prof. Mdoe ameitaka Bodi ya
Wakurugenzi wa AMGC kutimiza wajibu wake muhimu katika kusimamia na
kuendeleza Kituo hicho ambacho kina mchango mkubwa katika utafiti na
uongezaji thamani ya madini.
“Wizara yangu itajitahidi
kuhakikisha kuwa mpango kazi ambao tumeuidhinisha leo, unatekelezwa
ipasavyo na kwa wakati kadiri tulivyokubaliana,”alisema Prof. Mdoe.
Akitilia mkazo maagizo ya Waziri
Mkuu, Prof. Mdoe amesema kuwa yale ambayo yalisemwa na Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa yatekelezwe. Maeneo hayo ni pamoja na nchi wanachama
kulipa ada na michango yao kwa wakati, AMGC kupewa ithibati ili kiweze
kutoa huduma zake kwa viwango bora na vinavyokubalika kimataifa, nchi
wanachama kutumia huduma za kituo kwa ukamilifu na kutangaza kazi na
huduma za kituo ili kuvutia sekta binafsi kutumia huduma hizo.
Kwa kufanya hivyo kituo
kitaimarika kifedha na kuacha utegemezi wa michango ya wanachama
kujiendesha ikizingatiwa kuwa sasa kimepanda hadhi na kuwa cha Afrika
nzima badala ya nchi nane wanachama wa sasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati
na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Lokeris Peter amesema kuwa Bara la
Afrika linatakiwa kuvutia wawekezaji katika sekta ya Madini kwa ajili ya
kuleta maendeleo endelevu.
Lokeris amesema kuwa Madini ni sekta ambayo inaweza kuziendeleza nchi za Kiafrika kiuchumi ikitumiwa na kusimamiwa vizuri.
“Tusisahau kuendeleza jamii
inayozunguka maeneo ya migodi ya Madini, tuwafanye wajisikie kuwa sehemu
ya wanufaika wa raslimali hizo muhimu zipatikanazo kwao,”alisema
Lokeris.
Katika Mkutano huo Sudan imechaguliwa kuwa Makamu Mwenyeki huku Uganda ikichukua nafasi ya Ukatibu.
Mkutano huu umemalizika leo hadi mwakani utakapofanyika Sudan chini ya uenyekiti wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment