Wednesday 20 September 2017

Mahakama yamtaka Kitilya na wenzake kuwa na subira




Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake wawili kuwa na imani pamoja na subira dhidi ya upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili kwa kuwa unakaribia kufika mwisho.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha amesema hayo  leo asubuhi kesi hiyo ilipofika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa huku upande wa Jamhuri ukidai kuwa upelelelezi bado haujakamilika.
Kabla ya Hakimu Mkeha kusema hayo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Mutalemwa Kishenyi ulidai kuwa, mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa waliomba siku 14 ili waweze kuelezea Hali ya upelelezi dhidi ya kesi hiyo lakini muda walioomba haujawatosha kukamilisha malengo hayo hivyo wakaomba kuongezewa siku 14  ili kukamilisha na waje kueleza hali ya upelelezi.
"Mheshimiwa tunafanya jitihada kuona upelelezi unakamilika, tunaomba tuongezewe muda wa siku 14" amedai Kishanyi.
Hata Hivyo jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na wakili Masumbuko Lamwai amedai "kesi hiyo imekuwa kama ya kukomoana komoana", akaongeza kudai kuwa, Wateja wao wamekaa gerezani kwa takribani mwaka mmoja na nusu kwani kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa walifikishwa mahakamani Aprili Mosi mwaka jana.
 Amedai uchunguzi katika mashtaka dhidi ya Wateja wao unahusu nyaraka ambazo upande wa mashtaka wanazo na hakuna uchunguzi zaidi ya nyaraka.
"Shtaka la utakatishaji wa fedha dhidi ya washtakiwa limewekwa kwa makusudi ili washtakiwa waendelee kukaa gerezani, kwa mtu aliyekaa gerezani kwa takribani mwaka mmoja na nusu ukimwambia upelelezi bado inaleta mshangao.
Amesema, washtakiwa ni watu wazima wanashughuli zao ambapo zingine zimefilisika kwa kukosa usimamizi, " Tunajua mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi hii lakini upande wa mashtaka wanatumia vibaya taratibu za kimahakama.

Akijibu hoja hizo, Hakimu Mkeha amewaambia washtakiwa kuwa upelelezi unaofanywa unakaribia mwisho, naomba muwe na imani, nimejiridhisha Mimi Jana kwa macho yangu kuwa upelelezi unakaribia kufika mwisho, tuwe na subira. Amesema Mkeha

Kitilya na wenzake, aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon wanashtakiwa kwa utakatishaji wa fedha dola milioni 6, kesi hiyo imeahirishwa hadi Octoba 5, 2017.

No comments:

Post a Comment