Wednesday 20 September 2017

TCRA imetoa Tahadhari kwa Watanzania kuacha kutumia vibaya mitandao ya simu na intaneti

               PIX 1                      
Kaimu Meneja wa Mawasiliano toka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Semu Mwakyanjala akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea matumizi sahihi na salama ya mitandao ya kompyuta na intaneti mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Afisa Habari wa Idara ya habari (MAELEZO) Bi. Fatma Salum.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
                                                                                                                                                                 
                                                                                                                                                                                                
Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa rai kwa Watanzania kuacha kutumia vibaya mitandao ya simu na intaneti badala yake waitumie kwa ajili ya kurahisisha harakati zao za kujiletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bw. Semu Mwakyanjala wakati akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
Mwakyanjala alisema kuwa licha ya teknolojia ya mawasiliano kukua na kuleta faida kwenye jamii yetu, bado kuna changamoto nyingi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anatumia vizuri mitandao hiyo kwa faida yake na taifa kwa ujumla.
“Kutokana na mabadiliko ya kila siku ya teknolojia hasa kwenye sekta ya mawasiliano imesababisha baadhi ya watu kutumia vibaya teknolojia hiyo kupitia mitandao ya kompyuta na intaneti kufanya uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo wizi, utapeli, ulaghai na uchochezi,” alieleza Mwakyanjala.
Pia alibainisha kuwa wapo baadhi ya watu wasiokuwa wazalendo ambao hutumia mitandao hiyo kusambaza taarifa zenye maudhui ya chuki au uchochezi na kuongeza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria .
Mwakyanjala alisema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kusimamia usalama mitandaoni kupitia Kitengo cha Dharura cha Kuitikia Matukio ya Usalama Kwenye Mitandao (TZ-CERT) ambacho kinafanya kazi ya kuratibu matukio ya usalama katika mitandao ya kompyuta na intaneti kwa kushirikiana na vyombo vingine husika vya kikanda na kimataifa.
Akieleza mambo muhimu ya kuzingatia kwa watumiaji wa huduma za mitandao, aliwataka watumiaji hao kuwa makini na taarifa zao binafsi wanazoweka kwenye mitandao ya kijamii pamoja na kutumia program za kujikinga na virusi hatarishi katika kompyuta na simu zao.
“Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba anajilinda na uhalifu wa mitandaoni na kuepuka kumtajia mtu mwingine taarifa zake binafsi kama vile neno la siri (password) kwani kufanya hivyo kunawarahisishia watu wenye nia mbaya kufanya uhalifu,” alisisitiza Mwakyanjala.
 
Aidha alibainisha kuwa matumizi ya mtandao yamepanuka sana nchini ambapo  kwa sasa Tanzania kuna watumiaji wa mtandao wanaokadiriwa kufikia milioni 18 ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na watumiaji milioni 5 tu.  
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilianzishwa mwaka 2003 kwa sheria na. 12 kwa lengo la kusimamia na kudhibiti mawasiliano ya kielektroniki na huduma za posta.

No comments:

Post a Comment