Sunday 24 September 2017

Bilioni 15 Zahitajika Kujenga Mfumo wa Maji Taka Manispaa ya Tabora

TUWASA 4
Na. Tiganya Vincent – RS-Tabora
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka katika Manispaa ya Tabora inahitaji jumla ya shilingi bilioni 15 kwa ajili ya hatua za awali za ujenzi wa mtandao wa kuondoa maji taka katika maeneo mbalimbali mjini humo.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA, Bwire
Mkama wakati wa uzinduzi wa Malipo kabla ya matumizi ya maji ili kukabiliana na wadaiwa sugu na wateja ambao upenda kutumia maji bila kulipia huduma hiyo kwa wakati.
Alisema kuwa lengo ni kutaka kuwa na miundo mbinu itakayosaidia kuondoa maji taka katika majumba ya watu na mitaa kwa ajili ya kupeleka sehemu ambayo yatawekwa pamoja ili kuiepushia jamii na maradhi yanaweza kusababishwa na kuzagaa kwa maji hayo.
Bwire alisema kuwa Bodi ya TUWASA iliona umuhimu kwa kuanza mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya shughuli hiyo.
Alisema kuwa hivi sasa wameshaandika andiko la uwekezaji katika mtandao wa maji taka na kulipeleka Wizarani kwa ajili ya kutafuta fedha za kutekeleza mradi huo.
Bwire alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo mapema kwa sababu upatikanaji wa maji safi na salama unapoongezeka katika miji ndivyo maji taka nayo yanavyoongezeka.
Alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusaidia kusukuma andiko lao ili fedha ya utekelezaji wa mradi huo iweze kupatikana na kazi ianze mara moja.
Alisema kuwa hivi sasa TUWASA ina jumla ya kilometa 20 tu za mtandao wa maji taka katikati ya mji wa Tabora ambapo ni asilimia 6 tu ya wakazi wa Manispaa ya Tabora ndio wameunganishwa katika huduma hiyo.
Aidha alisema kuwa hivi sasa wanashirikiana na Manispaa ya Tabora ili kuanisha maeneo ambayo wanaweza kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji taka.
Kwa mujibu wa Bwire, mabwawa yaliyopo hivi sasa hajatoshi kutokan na ongezeko kubwa la uzalishaji wa maji taka.
 
Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alikubali kushirikiana na TUWASA katika kuhakikisha andiko hilo linafanikiwa na mradi unaanza ili kuboresha huduma hiyo na kuepusha jamii na magonjwa.

No comments:

Post a Comment