Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali itaendelea kutoa fedha
zaidi za Bajeti kwa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya kipaumbele kwa
kadri inavyoendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa wakati akiahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
“Serikali inaendelea kusimamia kwa
karibu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2017/2018, aidha mwenendo wa
utekelezaji unaridhisha. Serikali imeweka jitihada kubwa za kuimarisha
ukusanyaji mapato ya ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki”
amefafanua Waziri Mkuu.
Katika hatua hiyo Mhe. Majaliwa
ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti, 2017 Serikali
imetoa jumla ya Shilingi Trilion 3.944 zinazotokana na mapato ya ndani
na fedha za nje kwa matumizi ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi
ya maendeleo, ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma na Deni Taifa.
Aidha, Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa
Serikali itahakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya nchini
kinakuwa na vifaa vya kutosha ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Hali ya upatikanaji wa dawa,
vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya
nchini imeendelea kuimarika” ameongeza Mhe. Majaliwa.
Akizungumzia suala la elimu,
Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea na mpango wa Elimu bila malipo
kwa kupeleka fedha moja kwa moja katika shule za Umma za Msingi na
Sekondari nchi nzima.
Kwa upande wa Kilimo Waziri Mkuu
amesema kuwa, Serikali imeamua kuanza kwa kuweka mkazo wa kuyaendeleza
kwa kasi mazao makuu matano ya biashara yakiwemo Pamba, Tumbaku,
Korosho, Chai na Kahawa.
Waziri Mkuu ameahirisha rasmi Bunge la Jamburi ya Muungano wa Tanzania mpaka Novemba 7, 2017.
No comments:
Post a Comment