Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi
wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 limeitangaza
Clouds Media Group kuwa mshindi wa Tuzo hiyo kwa mwaka 2017.
Tuzo hiyo imetolewa Umoja wa
Klabu za Waandishi wa Habari nchini UTPC wakati wa mkutano wake mkuu wa
unaofanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort mkoani Tanga.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa uongozi wa Clouds Media Group na Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura.
Mbali na kupewa tuzo hiyo,pia
Clouds fm imekabidhiwa hundi ya shilingi milioni 10 kama pole kwa
changamoto waliyopitia baada ya kituo cha matangazo kuvamiwa na mkuu wa
mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda aliyekuwa ameambatana na askari
polisi.
Mwenyekiti wa Jopo la Majaji
Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka
2017,Jenerali Ulimwengu alisema madhumuni ya tuzo ya mwangosi ni
kumuenzi na kumkumbuka kwa kumpa mwanahabari au chombo cha habari tuzo
yenye jina lake.
“Jopo la majaji mwaka huu
tunaitangaza Clouds Fm kuwa mshindi wa tuzo ya Daudi Mwangosi mwaka 2017
kwa sababu tarehe 17,Machi,2017 wanahabari wa Clouds walivamiwa na mkuu
wa mkoa wa Dar es salaam akiwa na askari polisi akiwataka kutangaza
habari ambayo hawakuitaka lakini wafanyakazi hao wakakataa kutangaza
habari hiyo,huu ni ushujaa kwani hawakukubali kutii amri ambazo zilikuwa
kinyume na kazi waliyofundishwa na uandishi wa habari”,alisema Ulimwengu.
“Lengo la tuzo hii
iliyoanzishwa mwaka 2013 na UTPC ni kupinga vitendo viovu wanavyofanyiwa
waandishi wa habari , hutolewa kwa mwandishi wa habari anayefanya kazi
nchini aliyekutana na madhila katika utendaji kazi wake ama chombo cha
habari ambacho kimekutana na madhila”,alieleza Ulimwengu.
Aliongeza kuwa tuzo hiyo inalenga kuwafanya wadau wa habari ikiwemo serikali kutambua kazi ya waandishi wa habari.
“Daudi Mwangosi alikuwa
mwenyekiti Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa,aliuawa Tarehe 2
mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo mkoani humo,akitekeleza majukumu
yake,ni mwandishi wa habari wa kwanza nchini Tanzania kuuawa akiwa
kazini, kifo chake kilishtua na kusikitisha watu wengi duniani”,alieleza.

Mkurugenzi wa Tanzania Media
Foundation,Ernest Sungura akikabidhi tuzo Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa
na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa Afisa Mahusiano kutoka
Clouds Media Group Simalenga Simon

Mkurugenzi wa Tanzania Media
Foundation,Ernest Sungura cheti cha ushindi kwa Afisa Mahusiano kutoka
Clouds Media Group Simalenga Simon

No comments:
Post a Comment