Wednesday 6 May 2015

Waathirika wa mvua wasaidiwe - Maalim Seif.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameiagiza Idara ya Maafa Zanzibar kushirikiana na wakuu wa wilaya kufanya utafiti juu ya watu walioathiriwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha ili wapatiwe misaada ya haraka.
 Alisema mvua hiyo imeleta athari kubwa kwa baadhi ya wananchi hasa katika maeneo ya Mjini na Magharibi na wanahitaji misaada ya haraka.
 Maalim Seif alitoa agizo hilo wakati akifanya ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo yakiwamo Mwanakwerekwe, Kwahani na Jang’ombe ambako baadhi yao hawana makazi.
Pia Maalim Seif alisema upo umuhimu kwa Baraza la Manispaa na Idara ya Ujenzi kufanya utafiti wa kina juu ya hali ya mitaro katika Manispaa ya Zanzibar ikiwa ni njia moja wapo ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la kupita na kutuwama kwa maji katika maeneo hayo. 
Alitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyoathirika na mvua hasa yale yaliyo karibu na maziwa, kuchukua tahadhari hasa kwa watoto ambao hupenda kucheza kwenye maeneo hayo bila  kujua athari zinazoweza kujitokeza.
 Akiwa katika eneo la bwawa la Mwanakwerekwe, Maalim Seif alielezwa kuwa kijana Hamad Juma Suleiman (26), mkazi wa Mwanakwerekwe, alizama na mpaka sasa hajaonekana, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alikitaka kikosi cha zimamoto na uokozi kuendelea kumtafuta mtu huyo ili stiriwa.
 Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Gora Haji Gora, alisema wanaendelea kumtafuta kijana huyo licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo vumbi jingi litokanalo na takataka katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, alisema serikali iko pamoja na waathirika hao na inaendelea na taratibu zake ili iwapatie misaada inayohitajika.
Familia zaidi ya 200 zaathriki na mvua Zanzibar.

No comments:

Post a Comment