Sunday 10 May 2015

Malori yenye mahindi yakwama mpakani mwa Tanzania, Kenya

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Zaidi ya malori 50 yenye shehena za magunia ya mahindi  yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nchini Kenya, yamekwama kwa zaidi ya siku tatu sasa katika mpaka wa Sirari na kusababisha  msongamano mkubwa katika barabara kuu.
 
Kitendo hicho kimelazimisha baadhi ya malori hayo kushusha shehena za nafaka hizo na kuvushwa kimagendo kupitia njia za panya kwenda Kenya na kuisababishia Serikali ya Tanzania kukosa mapato yake.
 
Hali hiyo imeelezwa kuwa inachangiwa na urasimu na migogoro  ya kiutendaji ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara eneo la Sirari, kuwapo kwa mawakala wawili wanaotoza ushuru wa mazao na uwapo wa maofisa wa kilimo katika kituo hicho kwa zaidi ya miaka 10.
 
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na wananchi wilayani Tarime, wamemuomba Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira (pichani), kuwaondoa maofisa kilimo waliohudumu katika kituo hicho kwa zaidi ya miaka 10 kwa madai kwamba wanachangia kuzorota kwa makusanyo ya mapato katika kituo hicho ambapo hufanya kazi kwa mazoea.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari katika mji mdogo wa Sirari juzi, baadhi ya wafanyabiashara wanaosafirisha nafaka walidai kuwa malori hayo yenye shehena ya magunia ya mahindi yamekwama kuvuka mpaka kwenda Kenya licha ya kuwa na leseni na vibali vya kusafirishia nafaka hizo.
 
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Gimonge Nyagwisi, alisema hali hiyo inachangiwa na baadhi ya maofisa Idara ya Kilimo katika kituo cha Forodha Sirari, kuhudumu hapo kwa zaidi ya miaka 15. 
 
Mbali ya Nyagwisi, baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na NIPASHE kuhusu suala hilo ni Nyamorea Ndera, Samwel Sabai, John Kisiri, Mabula Makoye, Mushi Alex, Joyce John, Onyango Okelo, Thomas Andrew, Mashimba Madoho, Matiko Lameck na Yakobo Masafa.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Athuman Akalama, alipotafutwa ofisini kwake na kwa njia ya simu, kuzungumzia suala hilo, hakupatikana.
 
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Beredia Balozi, alisema yeye si msemaji na kueleza kwamba bosi wake amesafiri kikazi kwa takriban mwezi mmoja sasa.

No comments:

Post a Comment