Sunday 10 May 2015

MAONI: Athari za mafuriko Dar ni za kujitakia






Maji yakiwa yamefurika katika nyumba zilizopo eneo la Jangwani jana kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam. Picha na Salim Shao

Tangu juzi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake wamekuwa katika wakati mgumu kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilishatoa taarifa kuwa mvua hizo zingeendelea kwa siku kadhaa.
Mvua kubwa katika jiji hili siyo tukio geni, ni tukio la kila mwaka na kwa kawaida huambatana na mafuriko katika maeneo mbalimbali.
Mafuriko hayo nayo aghalabu huwaacha wakazi wa jiji hili katika majonzi kutokana na  kukosa makazi hasa kwa watu waliojenga mabondeni,  kusitisha biashara kwa wafanyabiashara na hata kuwapo kwa vifo au watu wanaopatwa na majeraha.
Aidha, mafuriko katika jiji hili huathiri matumizi ya barabara kadhaa muhimu kwa watu wanaotumia vyombo vya usafiri.
Kwa sababu hii usafiri kwa wanafunzi na hata wafanyakazi hugeuka adha kubwa kiasi cha kuathiri ufanisi wao kazini.
Kwa ufupi, katika jiji hili, mvua kubwa inaponyesha hata kwa muda mchache, shughuli nyingi muhimu husimama na hatimaye kuathiri maendeleo ya jiji hili tegemeo kwa uchumi wa nchi.
Pamoja na athari hizi zinazojirudia kila mwaka, tunalazimika kupaza sauti kwa mara nyingine tukizinyooshea kidole mamlaka husika kwa kushindwa kulinusuru jiji hili na athari za mvua hizo.
Tumesema mara kwa mara na tunaendelea bado kusisitiza kuwa majanga yatokanayo na mvua katika jiji la Dar es Salaam, kwa kiwango kikubwa ni ya kujitakia. Ukweli kuntu ni kuwa baadhi ya wakazi hawapo makini, lakini mamlaka husika nazo zimelala usingizi wa pono.
Wapo wakazi  wanaojitakia madhara kwa kung’ang’ania kuishi katika maeneo hatarishi ambayo mengi yapo mabondeni.
Tunawatanabahisha wakazi hawa kuwa kuendelea kuishi katika maeneo haya ni sawa na kujilipua.
Kwa upande mwingine, mamlaka katika jiji hili kama  Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dawasa na vyombo vingine vya Serikali, vimeshindwa kulisaidia jiji kuondokana na adha hii.  Siku zote tunachokisikia kutoka kwa viongozi ni kauli za kuwataka wakazi wa mabondeni kuhama. Hatujasikia kuwapo kwa mpango mkakati wowote wa kuzuia athari za mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Mathalani wakati mara zote viongozi wakitoa kauli za watu kuhama mabondeni, kasi ya ujenzi katika maeneo hayo bado inaongezeka na hatujaona juhudi thabiti za kuwahamisha wakazi hao zaidi ya kuwapa stara wanapokumbwa na matatizo.
Matatizo ya mafuriko katika jiji hili hayaishii kwa watu wanaoishi mabondeni. Hatujaona juhudi za kitaalamu zikichukuliwa kunusuru maeneo mengine ambayo nayo huleta adha kubwa kwa wakazi.
Iko mifano kadhaa ya maeneo katika barabara muhimu jijini ambazo hugeuka kero kubwa wakati wa mvua kubwa. Maeneo hayo ni kama Vingunguti, Tazara, TMJ hospitali na barabara ya Bibi Titi Mohamed.
Tunauliza; tunawezaje kulipa jiji hili hadhi ya ukubwa katika nchi ikiwa tunashindwa kuwa na mifumo imara ya mifereji ya  kusafirisha maji?
 Kwa nini mamlaka ziendelee kuruhusu ujenzi wa makazi hata katika maeneo ambayo ni mapitio ya maji kama ilivyo maeneo ya Mikocheni na Msasani? Mamlaka husika hazina budi kuamka na kuchukua hatua sasa kabla hayajatokea madhara makubwa.

No comments:

Post a Comment