Saturday 2 May 2015

Wafanyakazi Dar waomba wapunguziwe kodi.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
 
Wafanyakazi mkoa wa Dar es Salaam, wameiomba serikali kuwapunguzia kodi kwa asilimia tisa kutokana na mishahara midogo wanayopata inayowaongezea ugumu wa maisha.
Walitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika kimkoa. Sherehe hizo ziliambatana na maandamano kuanzia viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Uwanja wa Taifa na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
 
Maandamano hayo ya taasisi, mashirika na makampuni mbalimbali mara baada ya kuwasili ndani ya viwanja hivyo yalionyesha shughuli wanazofanya.
 
Akizungumza kwenye sherehe hizo, Katibu wa chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi nyinginezo (Tamico), Charles Mgashi, alisema kodi ambazo wanataka serikali izipunguze ni zile zinazokatwa kwenye mishahara kila mwezi.
 
Pia wafanyakazi hao wameitaka serikali kuondoa kodi katika mafao ya kustaafu na kodi ya mapato yatokanayo na mshahara baada ya kuondoa ya lazima. Mgashi alisema lipo tatizo sugu ambalo baadhi ya taasisi za umma na za watu binafsi zinakwepa kutekeleza sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004. Alisema sheria hiyo inataka kushirikishwa kwa wafanyakazi kupitia mabaraza ya wafanyakazi kupitisha bajeti ya taasisi zao.
 
Aidha, kutokana na tatizo hilo wameitaka serikali kupitia Bunge kutopokea bajeti za taasisi za umma zilizopelekwa bungeni bila kuzingatia sheria hiyo.
 
Waliitaka serikali iboreshe mazingira ya kufundishia kwa walimu kwa kuweka vitendea kazi, vitabu na madarasa ili ufaulu uendelee kuongezeka.
 
Kadhalika kutafuta ufumbuzi wa madeni mbali mbali ya wafanyakazi yanayotokana na likizo, uhamisho, mafunzo ya kukaimu madaraka na kukemea  baadhi ya waajiri wasiotambua vyama vya wafanyakazi hususan sekta binafsi. “Lipo tatizo la unyanyasaji wa wazawa kwenye baadhi ya makampuni ya nje hapa Tanzania ambayo wafanyakazi wake hufanya kazi kwa saa 16, kampuni hizi zinaajiri wageni na kuwalipa mishahara midogo wazawa,” alisema. Wakati wafanyakazi hao wakilia na serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki, aliwakumbusha wafanyakazi wanapodai haki wajiulize suala la uwajibikaji kama wanalitimiza.
 
Pia alisema wajibu wa kila mfanyakazi ni kufanya kazi yenye tija kwa saa nane na kama mtu hafanyi hivyo ni fisadi na mfilisi uchumi. Kuhusu kupunguziwa kodi ya mapato inayotozwa kwenye mishahara na mlolongo wa kodi, Sadiki aliwaahidi wafanyakazi kulifikisha kwenye mamlaka husika ili ilifanyie kazi.

No comments:

Post a Comment