Saturday 2 May 2015

Selcom inayouza Luku yatishia kuishtaki serikali.


Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
 
Kampuni ya Selcom iliyoingia mkataba na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuuza umeme kwa njia ya mtandao, imesema Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amekurupuka kuvunja mkataba kati yake na Tanesco na kutishia kuishitaki serikali.
 
Kampuni hiyo imesema serikali  imepata hasara ya Sh. bilioni 6.0 katika kipindi cha siku nne, ambacho kampuni hiyo ilisitishwa kutoa huduma ya kuuza umeme. Kampuni hiyo ilisema huuza umeme kwa asilimia 75.
 
Aidha, kampuni hiyo imesema haijapata notisi toka serikalini ya kusitishwa kwa mkataba wake na Tanesco.
 
Juzi waziri Simbachewene alitangaza kusitisha mkataba na kampuni hiyo kwa kushindwa kutoa huduma bora ya mfumo wa Luku kutokana na mitambo yao kutokukidhi vigezo na kusababisha usumbufu kwa wateja.
 
NIPASHE Jumamosi ilifanya mahojiano na Meneja Ukuzaji Biashara na Masoko kutoka Kampuni ya Selcom, Juma Mgoli, ambaye alisema ameshangazwa na taarifa ya waziri kudai kampuni yake haina vigezo wakati imekuwa ikiuza umeme wa Tanesco kwa asilimia 75.
 
Alisema wameshindwa kuelewa ni vigezo gani vilivyotumiwa na waziri kusitisha mkataba, wakati kampuni yake imekuwa ikiuza umeme wa Sh. bilioni 1.0 hadi bilioni 2.0 kwa siku.
 
Aliongeza kuwa inapokaribia mwisho wa mwezi mauzo hufika hadi Sh. bilioni 4.0  kwa siku.
 
Alisema kutokana na mauzo hayo, inaonyesha dhahiri kuwa kampuni yao inafanya vizuri sokoni na kwamba tatizo la mtandao halipo upande wao bali lipo kwa Tanesco.
 
Alisema Tanesco ina mashine za Electronic Vending Getway (EVG) ambazo uwezo wake ni mdogo katika kuhudumia wateja, hivyo kusababisha ukosefu wa mtandao. “Mfano mzuri nadhani unaona tangu tumeacha kutoa hiyo huduma kuna foleni kubwa kwenye vituo vinavyouza umeme sasa, tutaambiwaje hatufanyi vizuri sokoni,” alihoji. 
 
Aliongeza kuwa Selcom imejiunganisha kwenye benki 34 kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
 
 Alisema toka kampuni yake ilipozuiwa kuuza umeme katika kipindi cha siku nne, Tanesco imepata hasara ya Sh. bilioni 6.0 na serikali imepoteza mapato ya kodi ya zaidi ya Sh. bilioni 1.0.
 
Hata hivyo, alisema suala hilo linahusu masuala ya kisheria na kwamba wameshawasiliana na wanasheria wao kuangalia kama kuna ukiukwaji wowote wa mkataba huo ili sheria ichukue mkondo wake.
 
Alisema waziri hana mamlaka ya kuvunja mkataba kienyeji kwani uvunjaji wa mkataba una utaratibu wake.
 
Usitishwaji wa huduma hiyo, ulianza tangu mwanzo wa wiki hii ambapo juzi baadhi ya wateja walikuwa wakitumia ujumbe mfupi kwenye simu zao za mkononi unaosema: "Ndugu mteja huduma ya Luku haipatikani kwa sasa kutokana na shida iliyopo upande wa washirika wetu, tafadhali tembelea wakala wa Tanesco kununua umeme wako".
 
Hata hivyo, jana wakati gazeti hili likielekea mtamboni ujumbe mwingine kupitia simu za mkononi  ulitumwa ukieleza: "Ndugu mteja sasa unaweza kununua umeme wako wa Tigopesa kwa kupiga namba *150* 01#
 
NIPASHE ilishuhudia vituo vingi vinavyouza umeme wa Luku vikiwa na foleni ya wateja wanaotaka huduma hiyo.
 
Baadhi ya wateja walikuwa wakiilalamikia Tanesco kuifungia kampuni iliyokuwa ikitoa huduma hiyo kwa njia ya mtandao na kusababisha usumbufu mkubwa.

No comments:

Post a Comment