Sunday 3 May 2015

KATIBA MPYA: Wingu linavyogubika hatima Mchakato wa Katiba Mpya


Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (kulia), wakizindua nakala za Katiba Inayopendekezwa.Picha ya maktaba  

Sheria hazielezi nini kitafuata baada ya kuahirishwa Kura ya Maoni, hivyo kufanya mchakato mzima sasa kutegemea utashi wa wanasiasa

Bado hakuna mwafaka kuhusu hatima ya Katiba Mpya, baada ya kuahirishwa kwa upigaji Kura ya Maoni iliyopaswa ifanyike Aprili 30 mwaka huu.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakisema Kura ya Maoni itafanyika wakati wowote mwaka huu baada ya kukamilika uandikishaji wapigakura kwa Mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR), wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani, wanaamini kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni, kungetoa fursa ya mchakato huo kurudi kwenye Bunge la Katiba.
Wapinzani hao wanasema hili litasaidia kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa Bunge la Katiba ambako kundi hilo lilisusa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo, wapo wanaoamini pia kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni, ndiyo mwisho wa Mchakato wa Katiba Mpya, hasa baada ya rais aliyeanzisha mchakato huo kumaliza muda wake baada ya uchaguzi mkuu.
Nec iliahirisha Kura ya Maoni iliyopaswa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kutokana na kulegalega kwa shughuli ya kuandikisha wapigakura kwa BVR na baada ya tamko hilo giza likagubika hatima ya mchakato mzima.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na mabadiliko yake yaliyofanyika mwaka 2012 na Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, ziko kimya juu ya nini kinafuata baada ya kuahirishwa kwa Kura ya Maoni.
Sheria hizo zimeeleza tu namna Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unavyopaswa kuendeshwa kuanzia siku ulipotangazwa hadi kupatikana kwa Katiba Mpya. Pia sheria zimeeleza nini kitafuata kama kura ya NDIYO haitafika zaidi ya 50 kutoka pande zote za Muungano.
Kifungu cha 35(3) cha Sheria ya Kura ya Maoni na Kifungu cha 36(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vinasema kama kura za ndiyo hazifiki zaidi ya nusu ya wapigakura wote Bara na Zanzibar, Tume ya Uchaguzi Nec, na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa makubaliano maalumu na baada ya tangazo la Serikali, watachagua njia nyingine ndani ya siku 30 tangu kutangazwa kwa matokeo hayo.
Ikifikia hapo mchakato wa upigaji Kura ya Maoni utaanza upya. Sheria zote zimempa Rais mamlaka ya kuitisha tena Bunge la Katiba kubadili vipengele vilivyokataliwa wakati wa upigaji kura.
Kifungu cha 35(5) cha Sheria ya Kura ya Maoni pamoa ja na Kifungu cha  36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vinasema, kama kura za HAPANA zitakuwa nyingi ikilinganishwa na kura ya NDIYO, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.
Vyama vya upinzani kupitia Umoja wao wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamekuwa wakitaka Kura ya Maoni iahirishwe ili kukaa na kutafuta kwanza mwafaka katika baadhi ya mambo ikiwamo Muundo wa Muungano.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa Ibrahim Lipumba, amesema siyo sahihi kuendelea na mchakato wa Kura ya Maoni, kabla ya kupitia upya maeneo yaliyoleta mpasuko kwenye Mchakato wa Katiba.
“Sisi tuligomea mchakato huo, pamoja na mambo mengine kutaka Serikali iuahirishe ili tumalize kwanza uchaguzi mkuu, halafu ndipo turudi kwenye Kura ya Maoni,” anasema Lipumba.
Kwa upande wake Mratibu wa Mtandano wa Kutetea Haki za Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Onesmo Olengurumwa anataka Kura ya Maoni isifanyike mwaka huu kwa sababu ya mazingira ya kisiasa yaliyopo.
“Serikali isijisikie kwamba imeshindwa katika hili. Nec iachwe ifanye kazi yake na mimi naamini kuwa kwa sasa kipaumbele cha kwanza cha Nec ni Uchaguzi Mkuu na siyo Kura ya Maoni,” anasema na kuendelea;
“Tunahitaji mwafaka wa kitaifa kuhusu suala la Katiba na tunaweza kufikia hatua hiyo kama wanasiasa wataamua kuwa na akili za kuaminiana bila kuwazia namna ya kutetea nafasi zao za kisiasa.”
Olengurumwa ambaye pia ni mwanasheria, amependekeza mabadiliko katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni ili kuwa na namna nyingine ya kushughulikia suala hilo.
“Watu wamekuwa wakilalamika kuhusu sheria hizo. Kwanza sheria zenyewe zimevunjwa mara kadhaa sasa tuzibadili kabisa ili tuwe na mjadala wenye afya kuhusu Katiba Mpya,” anasema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Benson Bana, anasema wapinzani na chama tawala CCM, wana tofauti kubwa katika suala la Mchakato wa Mabadiko ya Katiba.
Kwa mujibu wa Dk Bana, kuahirisha tu Kura ya Maoni, hakumaanishi kumaliza tofauti zilizopo. Bado kuna haja ya kukaa meza moja na kujadili tofauti hizo kwa faida ya taifa, anasema.
Dk Bana anasema haoni tatizo kama Kura ya Maoni itafanyika baada ya uchaguzi, na kwamba hofu kwamba tusipoifanya sasa huenda isifanyike tena haina msingi.
“Katiba Mpya siyo urithi wa Rais,  bali Rais ndiye anayepatikana kwa Katiba.
Hivyo Rais ajaye anaweza kuendeleza pale tulipofikia lakini hawezi kubadili wala kuusitisha mchakato wote,” anasema.
Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala anasema anaona kuna umuhimu wa wadau kukaa meza moja na kujadili tofauti zinazoonekana kwenye Mchakato wa Katiba, ikiwamo suala la kuwa na Tume huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na kupinga matokeo ya rais mahakamani.“Tunahitaji mambo haya kabla ya Uchaguzi Mkuu. Wapinzani wamekuwa wakiyapigia kelele kwa muda mrefu sasa. Naamini tukitekeleza hayo, Wapinzani hawatakuwa na cha kusema kama CCM itashinda,” anasema.


No comments:

Post a Comment