Sunday 26 April 2015

Azam, Simba kazi ipo


Zachuana kusaka mshindi wa pili, zinakutana Jumapili

Dar es Salaam. Kama ni ngoma, basi bado ni mbichi kwa Azam na Simba katika harakati zao za kuwania mshindi wa pili msimu huu.
Ushindi wa mabao 4-0 na 3-0 ambao timu hizo zilipata jana dhidi ya wapinzani wao, Stand United ya Shinyanga na Ndanda ya Mtwara umezidisha zaidi vita hiyo ya kuwania nafasi ya pili.
Pia, ushindi huo umeifanya mechi ijayo baina ya timu hizo mbili, Jumapili, Mei 3 iwe kama fainali, kwani ndiyo inayoweza kuamua nafasi hiyo itakwenda kwa nani.
Hata hivyo, Azam iliyofikisha pointi 45 dhidi ya Simba yenye pointi 41, ina mchezo pungufu ikilinganishwa na Simba, kitu pekee kinachoipa faida zaidi katika harakati zake za kusaka nafasi hiyo.
Katika mchezo wa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilianza kuhesabu bao lake la kwanza, mapema dakika ya nane kupitia kwa kiungo Jonas Mkude.
Bao hilo lilifuatiwa na mashambulizi makali kwenye lango la Ndanda, yaliyosababisha makosa dhidi ya Emmanuel Okwi na kusababisha penalti iliyopigwa na Ibrahim Ajibu aliyepaisha na baadaye Ramadhan Singano, Said Ndemla kupachika mengine mawili.
Ndanda ambao wako katika hatari ya kushuka daraja walishindwa kuhimili kasi ya washambuliaji wa Simba na hivyo mabeki wao kujichanganya kila mara wakati mwingine kumchanganya kipa wao, Salehe Malande aliyeonekana akiwafokea kila mara.
Simba walikwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao 3-0, lakini waliporudi kipindi cha pili walishindwa kufurukuta mbele ya Ndanda waliowabana vilivyo wasipate bao zaidi.
Nako kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam walijipatia mabao kupitia kwa Gaudence Mwaikimba (mawili), Brian Majwega na Farid Malick, yaliyotosha kuwapa pointi tatu muhimu mabingwa hao watetezi.
Kwenye Uwanja wa Sokoine ,wenyeji Mbeya City waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar,mabao yaliyofungwa na Rafael Alpha kwa penalti, dakika ya 45 baada ya kipa wa Kagera, Agatony Anthony kumfanyia madhambi Cosmas Fred wakati akielekea kufunga. Bao la pili la Mbeya City, liliwekwa kimiani dakika ya 56 na Deus Kaseke.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 52, inajiandaa kutwaa ubingwa kesho, Jumatatu dhidi ya Polisi Morogoro ikishinda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Imeandikwa na Charles Abel na Oliver Albert(Dar), Godfrey Kahango, Mbeya

No comments:

Post a Comment