Sunday 26 April 2015

Dk Hoseah awanyatia wagombea urais CCM

Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hosea

Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini wameeleza kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko hayo.
Dar es Salaam. Wakati viongozi wajuu wa CCM wakiendelea kulalamikia makada wanaowatuhumu kutumia fedha kujifagilia njia ya urais, mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema taasisi yake inakusanya taarifa zote za wanachama wa chama hicho tawala wanaotuhumiwa kutumia mlungula.
Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini wameeleza kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko hayo.
Jumatano, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata mwaliko wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia rushwa ndani ya chama hicho kwani rushwa inayoendelea kwa sasa iko wazi.
“Kazi ya kuwafuatilia imeshaanza muda mrefu, tunazo taarifa zao za kutosha kwa kila mwanasiasa anayelalamikiwa,” alisema Dk Hoseah wakati alipoongea na gazeti hili kuhusu sababu za taasisi yake kukaa kimya wakati ikielezwa hadharani kuwa rushwa imezidi katika harakati za uchaguzi ndani ya CCM
Dk Hoseah alisema kwa muda mrefu Takukuru imekuwa ikifuatilia mienendo ya wanasiasa wanaotaka uongozi kupitia chama hicho na ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema Takukuru kwa sasa inaendelea na kazi yake ya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo huku ikikusanya taarifa za kila mwanasiasa anayeonekana kutuhumiwa na vitendo vya rushwa.
“Siyo kwamba Takukuru haijaona wala haisikii malalamiko ya viongozi CCM. Tunajua wajibu wetu na kazi ya kuwafuatilia imeshaanza,” alisema Dk Hoseah.
“Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 imekataza wazi kwamba, ni makosa kutoa chochote kama zawadi kwa kundi la watu, vinginevyo ni kukiuka sheria hiyo. Labda kama anaonekana kuwa na fedha nyingi basi ajenge hata barabara kuliko kufanya hivyo.”
Dk Hoseah aliongeza kuwa sheria pia inazuia kuanza kampeni kabla ya muda kupangwa rasmi na Tume ya Taifa (Nec), kwa hivyo muda wa kampeni utakapoanza, itarahisisha kukusanya taarifa zake na kuchukua hatua kwa wanasiasa hao.
“Kwanza ni kosa kufanya kampeni kabla ya muda, lakini pia ni kosa kutoa zawadi kama maji ya kunywa kama unafahamu kuwa wewe ni mwanasiasa utakayegombea. Sheria yetu ya Takukuru inaweka wazi pia kitendo hicho ni kosa,” alisema Dk Hoseah.
Mapema wiki hii, akiwa kwenye vikao vya ndani na viongozi wa chama hicho wa Dar es Salaam, makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangulla alisema fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama “kama maandazi”, zitakuwa kitanzi chao kwenye uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa wanachama hao watang’olewa.
Mbali na Mangula, wengine waliowahi kulalamikia rushwa ndani ya chama hicho ni mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete ambaye alitahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kukiuangusha chama.
Mangula amtaja mgombea
Wakati Dk Hoseah akisema hayo, Mangulla juzi alidokeza uwezekano wa chama hicho kuwatema makada sita ambao wamesimamishwa kujihusisha na uchaguzi kwa mwaka mmoja, akisema kuwa CCM itampitisha mgombea ambaye “amekidhi vigezo, kanuni na taratibu” zao.
Mangula alisema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake mkoani Dar es Salaam kwa kuongea na viongozi.
“Chama kitafuata taratibu zote husika bila kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa wanaotaka kuwania nafasi hiyo... wanachama wenye nia ya kugombea nafasi ya urais na nyingine wanapaswa kusubiri mpaka utaratibu wa kutangaza nia na kufanya kampeni utakapotangazwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chama,” alisema Mangula ambaye alisisitiza wanachama kuepuka makundi ya urais.
Waliopewa adhabu kwa kukiuka taratibu zinazozuia kuanza kampeni mapema ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ambao ni mawaziri wakuu wa zamani, Bernard Membe (waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba (Sayansi na Teknolojia), Steven Wasira (Kilimo na Chakula) na William Ngeleja.
Wafuasi wa wagombea hao wamekuwa wakishambuliana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, hali inayoonyesha wazi kuwapo kwa makundi.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa CCM wametakiwa kuwachukulia hatua wanachama wanaoeneza siasa za makundi zenye kuzua migogoro inayotishia umoja na mshikamano ndani ya chama hicho.
Mangula alisema wanachama wa CCM wanapaswa kufahamu kuwa mgombea atakayesimamishwa ndiye atakaye wakilisha chama na si kujiwakilisha yeye, hivyo wanapaswa kumuunga mkono.

No comments:

Post a Comment