Tuesday 14 April 2015

Kinamama wajawazito zaidi ya 70 waandamana hadi hospitali ya rufaa ya Dodoma wakilalamikia vitendo vya unyanyasaji.






Kinamama wajawazito wanaohudumiwa na kituo cha kusubiri kujifungua cha Chikande manispaa ya Dodoma wameandamana hadi hosipitali ya rufaa ya Dodoma wakilalamikia vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa na walinzi wa hosipitali hiyo  ikiwemo kugoma kuwafungulia milango pindi wanapopata uchungu hasa nyakati za usiku na kusababisha baadhi yao kujifungulia njiani.
 
Kinamama hao zaidi ya 70 wameamua kuchukua uamuzi huo ili kufikisha kilio chao kwa uongozi wa hosipitali ya rufaa ya Dodoma kufuatia wenzao wawili hivi karibuni kuzuiwa kuingia hosipitalini hapo na walinzi na kulazimika kujifungulia kwenye lango kuu la hosipitali na vichakani hatua ambayo wamedai inawadhalilisha na inahatarisha afya ya mama na motto.
 
Kufuatia sakata hilo uongozi wa hosipitali ukalazimika kuitisha kikao cha dharula na jopo la walinzi wa zamu waliokuwepo kwenye matukio hayo hali iliyozua malumbano makubwa baina yao huku wakirushiana mpira kati ya walinzi wa lango kuu na wale wa mlango maalum unaotumiwa na kinamana hao kuhusu kuhusika na matukio hayo ya unyanyasaji.
 
Akizungumza kwa niaba ya mganga mfawidhi wa hosipitali hiyo Dk.Nassoro Mzee muuguzi wa zamu aliyekuwepo wakati sakata hilo linatokea Cecilia Sanya amesema uongozi wa hosipitali umesikitishwa na kuwepo kwa matukio hayo na umeahidi kuchukua hatua kwa kampuni ya ulinzi inayofanya kandarasi ya ulinzi hosipitalini hapo ili kukomesha matukio ya namna hiyo.

No comments:

Post a Comment