Thursday 23 April 2015

Wasomi wapinga Sheria Makosa ya Mtandao, Takwimu.


Rais Jakaya Kikwete.
Wasomi na wananchi mbalimbali, wamemuomba  Rais Jakaya Kikwete, kutosaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 huku wakieleza kuwa kama utasainiwa watahamasisha wananchi kuupinga kwa kufanya maandamano ya nchi nzima mitaani.
 
Aidha, wamesema muswada huo ukisainiwa watatumia kama fimbo kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutokichagua katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
 
Walisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo uliowashirikisha wananchi, wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu na wahadhiri wa vyuo vikuu kujadili athari za Sheria ya Takwimu  ya mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015. 
 
Wakati wa Bunge la 19 lilohitimishwa Aprili Mosi, mwaka huu, miswada hiyo iliwasilishwa na serikali bungeni kwa hati ya dharura na kupitishwa na Bunge na sasa hatua inayofuata utapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kuisaini ili iwe sheria ianze kutumika.
 
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitilia Mkumbo, akizungumza katika mdahalo huo alisema miswada hiyo kama itasainiwa na Rais na kuwa sheria, itakuwa na athari kubwa kwa wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu.
 
Profesa Mkumbo alisema kwa mfano, Sheria ya Takwimu ikianza kutumika itarudisha nyuma kupata wanafunzi wa PhD kwa sababu masomo yao yanategemea sana kupata takwimu.
 
“Usalama mkubwa kuliko wote ni uhuru wa kupata taarifa, kutokupata taarifa sahihi kuna hatari,” alisema.Profesa Mkumbo alisema Watanzania wanapenda kulalamika tu vijiweni lakini hawachukui hatua na kwamba katika suala la muswada huu kuna haja kwa wananchi kuandamana mitaani ili Rais asisaini.   Ndigwa Ezekiel, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alieleza wasiwasi wake kama suala hilo likienda kupingwa mahakamani haki itatendeka kwa madai kuwa imeegemea upande wa serikali.
 
Wachangiaji wengine walisema kama miswada hiyo itasainiwa, hawataipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. 
 
Wakati wa Mkutano wa Bunge, serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na kueleza kuwa mtu akatayebainika kusambaza picha za ngono, miili ya watu waliokufa kwa ajali na usambazaji taarifa za siri za serikali, atatozwa faini ya Sh. milioni tano, kifungo kisichopungua miezi sita au vyote kwa pamoja. Hata hivyo, kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema Rais Kikwete atatafakari na kuchukua maamuzi sahihi kabla ya kuusaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015.
 
Pia amesema Rais Kikwete atasikiliza maoni ya wadau wengine pamoja na kutoa uzito unaostahili kabla ya kusaini muswada huo. 
 
Balozi Sefue aliyasema hayo alipozungumza na NIPASHE kuhusu malalamiko ya wadau ya kumtaka Rais Kikwete kutousaini muswada huo.
 
Alisema teknolojia ya mitandao inakwenda kwa kasi kuliko udhibiti wake, hivyo ni lazima kuwapo na usawa katika kudhibiti masuala ya kimtandao. Balozi Sefue alisema hakuna sheria ambayo itatungwa na kupendwa na watu wote, lazima kutakuwapo na baadhi ya watu watakaoipenda na wengine kuikataa.
 
“Rais lazima atatoa uzito unaostahili kwa muswada unaotoka bungeni. Lakini pia anasikiliza maoni ya watu wengine wanasemaje. 
 
Lakini katika kutoa maamuzi atatoa kwa uzito unaostahili tu,” alisema Balozi Sefue.
 
Aliongeza: “…sisemi kuwa hatasikiliza maoni ya watu. Lakini ninachotaka kusema ni kuwa muswada wowote unaotoka bungeni ni lazima upewe uzito unaostahili…”
 
Alisema duniani kote, Ulaya na Amerika, wanayo sheria ya kudhibiti masuala ya mitandao kutokana na kuwapo kwa uhalifu, ambao unailetea madhara nchi.
 
Balozi Sefue alisema kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo kwa kile anachokifikiria, lakini siyo vizuri kutumia lugha ya kumshinikiza Rais asisaini muswada huo.
 
Machi 31, mwaka huu, serikali iliwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, lakini ulipingwa na wadau kwa madai kuwa hawakushirikishwa na unalenga kudhibiti mawasiliano ya wananchi wenyewe kwa wenyewe.
 
Baadhi ya makosa yaliyoainishwa katika sheria hiyo, ni pamoja na kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana na utambuzi, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza picha za utupu za watoto.
 
Mengine ni unyanyasaji kwa kutumia mtandao, kuchapisha taarifa yoyote, ambayo itasababisha mauaji ya kimbari, uwongo na matusi ya kibaguzi, huku adhabu kali ikiwa ni faini ya Sh. milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono mtandaoni.
 
BUNGE
Alipoulizwa kama Bunge limekwishaupeleka muswada huo kwa Rais Kikwete, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema hawapaswi kusema kama umepelekwa au la kwa kuwa utaratibu huo ni wa ndani.
 
“Si utaratibu wetu kusema kama muswada umepelekwa kwa Rais kusainiwa au la kwa sababu ni utaratibu wa ndani. Hivi ulishawahi kusikia tumesema jambo kama hilo?” alihoji Dk. Kashililah.
 
Awali, alipotafutwa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuhusu suala hilo alimwelekeza mwandishi kuwasiliana na Dk. Kashililah kwa kuwa yeye ndiye anahusika zaidi na masuala hayo.
 
“Mimi niko jimboni, lakini ni vizuri umtafute Katibu wa Bunge kwa sababu yeye atakuwa anafahamu zaidi na ndiye anashughulikia zaidi mambo hayo,” alisema Ndugai.
 
Aliongeza: “ Kwani mna wasisiwasi kwamba, unaweza kukwama? Mimi naamini mpaka Bunge lijalo utakuwa umesainiwa. 
 
Naomba umuulize Katibu wa Bunge ndio atakueleza vizuri kwa kuwa mimi sipo siwezi kufahamu.”
 
Hivi karibuni makundi mbalimbali, zikiwamo asasi za kiraia, zilionekana kupinga muswaada huo na kumtaka Rais Kikwete asisaini mpaka pale sheria hhiyo itakaporudishwa bungeni kuondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na haki za binadamu kwa ujumla.
 
NIPASHE iliona nakala ya barua  iliyokuwa imeandikwa na asasi 53 kwenda  kwa Rais Kikwete kumtaka asisaini sheria hiyo.
 
 Barua hiyo ilisema sheria hiyo itaminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa wananchi kuwasiliana na kupashana habari endapo itasainiwa bila marekebisho.  
 
“Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa uhuru wa mawasiliano na matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, Jamii Forums, Twitter, blog… Kupitishwa kwa sheria hii bila kufanyiwa marekebisho kutasababisha Watanzania wengi kutiwa hatiani bila sababu, lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari nchini,” ilisomeka hivyo.
 
Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Elizabeth Zaya na Thobias Mwanakatwe

No comments:

Post a Comment