Sunday 12 April 2015

Serikali yakubali kutatua madai ya madereva kumaliza mgomo nchini.


Serikali imekiri kutatua madai ya madereva wa mabasi ya abiria na malori nchini ili kumaliza tatizo la mgomo wa madereva hao ambao umesababisha mamia ya abiria kushindwa kusafiri kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoani na nchi za jirani ikiwemo Kenya.
ITV ilifika katika kituo cha mabasi cha Ubungo jijini Dar es Salaam majira ya asubuhi na kushuhudia mabasi ya abiria yakiwa yameegeshwa ambapo baadhi ya abiria waliotegemea kusafiri wameeleza adha walizokutana nazo.
 
Baada ya madereva kuendelea kushikilia msimamo wao wa kugoma, baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwa wakipita na abiria katika barabara ya Morogoro walianza kufukuzwa na kundi la vijana ili kuwapiga huku matairi ya magari yakichomwa moto ili kuzuia magari kutumia barabara ya Morogoro.
 
Kurushiwa mawe kwa askari wa jeshi la polisi ilisababisha mabomu ya machozi kuanza kupigwa hewani hali iliyosababisha watu kukimbia ovyoovyo huku baadhi ya walemavu wakiishiwa nguvu.
 
Umati wa watu walikuwa katika eneo hilo waliendelea kuzuia magari ambapo jeshi la polisi ikamua kuongeza nguvu kwa kuleta magari ya maji ya washa washa, gari la jeshi la wananchi Tanzania lakini jitihada hizo zilipoonekana kushindwa kuondoa makundi ya watu ndipo mabomu yakaanza tena kupigwa.
 
Kamishna wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam alilazimika kufika katika kituo cha Ubungo akiongozana na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam ambapo baada ya madereva hao kulazimisha kuzungumza na mawaziri husika, kamishna Kova alifanikiwa kumpata waziri wa kazi na ajira Mh Gaudencia Kabaka ambapo kabla ya waziri kuzungumza viongozi wa madereva hao wakaeleza madai yao sita.
 
Mmoja wa viongozi hao akasema polisi wametakiwa kuthibiti askari wake ili wasiwaonee madereva barabarani.
 
Katika kumaliza mgomo huo kutoendelea, kamishna Kova akakiri kuthibiti askari wake kutoendelea kusumbua madereva huku waziri wa kazi na ajira Mh Kabaka akikiri kuingilia kati ili kumaliza madai ya madereva hao.
 
Baada ya waziri kuwaridhisha madereva hao, madereva walianza kuruhusu abiria kuingia ndani ya mabasi kwa ajili ya safari kuanza ikiwa ni majira ya saa7 na nusu mchana.

No comments:

Post a Comment