Monday 13 April 2015

JK aonya chokochoko za siasa kupitia dini


JK aonya chokochoko za siasa kupitia dini
Rais Jakaya Kikwete akimpongeza Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu wakati wa ibada ya kumweka wakfu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Parokia Mama Mwenye Huruma, Ngokolo mjini Shinyanga jana. (Picha na Freddy Maro).

RAIS Jakaya Kikwete amesema wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani baadaye mwaka huu, kumeibuka nyufa zinazojengwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na mashabiki wao ambao wanatumia tofauti za dini zilizopo nchini kwa uchu wa kuingia madarakani.
Kwa hali hiyo, amewaomba viongozi wa dini kuchukua hatua kwa kukemea tatizo hilo ili kuliponya taifa na changamoto hiyo aliyoita kuwa ni kubwa, hasa ukizingatia kuwa Tanzania haina historia ya kuuana wala kugombana kwa sababu ya tofauti za kidini na kikabila.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika sherehe za kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mteule wa Jimbo Kuu la Shinyanga, Liberatus Sangu katika Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo mjini hapa.
“Katika kipindi hiki tunachotakiwa ni kubadilika ili kutoingia katika maangamizi… tunaomba viongozi wa dini kuliponya taifa na changamoto hii kubwa ili tudumishe namna ya kuishi pamoja, kwani hatutaki kuingia kwenye ukabila wala udini,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa kama kisingizio ni Katiba Pendekezwa, alisisitiza kuwa masuala ya dini yamerekebishwa hivi sasa hakuna tatizo tena, hivyo kinachotakiwa ni Watanzania kuwa wamoja na kudumisha mshikamano.
Rais Kikwete pia alitumia sherehe hizo kuwataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kuachana na imani potofu ya kuua vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alionya kama mafundisho yao yakiwaingia vizuri wanajamii, ni dhahiri wataachana na imani kwamba, macho mekundu ya vikongwe si kigezo cha ushirikina, hali kadhalika watafuta imani kuwa viungo vya albano ni chanzo cha utajiri, vikitumiwa na waganga wa kienyeji kung’arisha nyota za wafanyabiashara na wanasiasa.
Akizungumza kwa hisia kali, Rais Kikwete alisema: “Yamekuwepo malalamiko mengi kuwa Serikali haifanyi kazi, lakini hivi sasa kuna watuhumiwa 11 waliokamatwa kwa mauaji hayo ila tayari watuhumiwa 16 wako kwenye orodha ya kunyongwa. “Kama tungekuwa hatufanyi kazi, hata hao tusingewakamata, Magereza yamejaa wahalifu na kila mara nimekuwa nikitoa msamaha.”
Alisema kusimikwa kwa Askofu Sangu kumekuja kwa wakati mwafaka, kwani anaamini atashirikiana na viongozi wengine wa dini kuiongoza jamii ili kuondokana na vitendo viovu na vya kikatili dhidi ya vikongwe na albino.
Alitumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kuhakikisha jamii inakuwa mahali pazuri pa kuishi.
Rais pia alilipongeza Kanisa Katoliki kutoa mchango mkubwa katika masuala ya elimu na afya kwenye jamii na akamtaka kiongozi huyo kuendelea kushirikiana na Serikali ili kama kuna upungufu atakaouona aeleze ili kanisa na Serikali wajue namna ya kuyatatua ili kuongeza kasi ya maendeleo.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Mwanza, Thadeus Ruwa’ichi alimueleza Askofu Sangu kuwa changamoto iliyopo katika eneo lake la kazi ni kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na vikongwe.
“Kama alivyolisema Rais Kikwete, kinachotakiwa ni kuendelea kutoa elimu na ushirikiano wa jamii, jimbo hili ni kubwa lakini tayari unao wasaidizi walio na moyo wa kutenda kazi. Jimbo hili lina waumini zaidi ya 300,000, lina mapadre 18 na jimbo zima lina wahudumu wa kipadre 70, watawa wa kiume wawili na watawa wa kike 70, mafrateli 19,” alisema.
Kwa upande wake, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Askofu Mkuu Francisco Padilla, alimpongeza Askofu Sangu kwa kukubali uteuzi huo, kwani umetokana na sala za waumini wa Mkoa wa Shinyanga.
Alitamtaka pia asitende kazi kwa manufaa yake, bali ashirikiane na viongozi wengine kuleta maendeleo na kuwafundisha waumini misingi ya kimaadili kwa njia ya ushirikiano ili kuweza kuondoa changamoto zilizopo.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alimkaribisha katika baraza hilo Askofu Sangu, akisema kanisa linafurahishwa na uteuzi wake kwani kazi yake imeonekana, hivyo sasa ana jukumu la kuwaongoza mapadri na kuwaunganisha wanajamii.
Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania kuanzia mwaka 2012 limekuwa wazi kutokana na kifo cha Askofu Aloysius Balina.
Kabla ya uteuzi wake, Askofu Mteule Sangu alikuwa ni Ofisa Mwandamizi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu mjini Vatican. Tangu kifo cha Askofu Balina, jimbo hilo lilikuwa chini ya uangalizi wa Askofu Ruwa’ichi.

No comments:

Post a Comment