Thursday 23 April 2015

TFF iongeze adhabu vitendo vya kishirikina.


katuni
Wakati soka la Tanzania likizidi kudidimia siku hadi siku, klabu kongwe nchini zimeshindwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kulea na kuendeleza vipaji na badala yake viongozi wake wameonekana kuwekeza zaidi katika imani za kishirikina.
Katika mchezo wa soka tunaamini ushirikina hauna nafasi, na kama ungekuwa unasidia basi mikoa inayodaiwa kuongoza kwa imani za kishirikina nchini kama Sumbawanga, Shinyanga na Kigoma ingekuwa ikiongoza kwa timu za Ligi Kuu ambazo zingepishana kwa kutwaa ubingwa kila msimu.
Lakini hata hivyo, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi msimu huu ndiyo kwanza mkoa wa Shinyanga umetoa timu ya Stand United inayoshiriki Ligi Kuu huku Sumbawanga na Kigoma zikiendelea kuwa watazamaji tu.
Kadhalika nchi kama Nigeria ambayo ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo zinatikisa kwa imani za kishirikina, timu yao ya Taifa, Super Eagle ingekuwa inatwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika (Afcon) kila mwaka, lakini msimu uliopita tulishuhudia ikishindwa hata kufuzu fainali hizo zilizofanyika Guinea ya Ikweta.
Tumelazimika kuyazungumza hayo kutokana na ukweli kwamba, licha ya Simba kupigwa faini ya Sh. 800,000 kwa kugoma kuingia vyumba vya kubadilishia nguo katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, kutokana na imani za kishirikina, wachezaji wa timu hiyo wakiongozwa na viongozi wao, Jumamosi walirudia tena vitendo hivyo jijini Mbeya.
Kabla ya mechi kuanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya, wachezaji wa Simba hawakuingia vyumbani kubadilisha jezi badala yake waliingia ndani ya basi lao na kuvalia humo.
Na baada ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza, wachezaji na benchi lote la ufundi la Simba walikusanyika kwenye benchi lao kwa kipindi chote cha robo saa ya mapumziko, kinyume cha Kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) toleo la 2014. 
Awali wakati wa kuingia uwanjani, kikosi cha Simba ndicho kilichokuwa cha kwanza kuingia kwenye Uwanja wa Sokoine majira ya saa 9:20 alasiri kwa miguu na kuliacha basi lao kubwa likiingia uwanjani likiwa na dereva na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo ya Msimbazi.
Lakini katika hali ya kushangaza, baada ya kuingia uwanjani, wachezaji wote wa Simba hawakwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo badala yake walikaa pembeni mwa uzio mdogo wa ndani ya uwanja wakisubiri maelezo kutoka kwa maofisa waliokuwa wametangulia.
Wakati timu zikiendelea kupasha, kulizuka mvutano mkubwa kati ya maofisa wa Simba na City, Simba wakitaka wakae benchi la kulia ambalo kwenye Uwanja wa Sokoine limekuwa likitumiwa na City ingawa kwa mujibu wa kanuni za Fifa timu ngeni ndiyo inayotakiwa kukaa upande huo.
Hata hivyo, Chama cha Soka cha Mbeya (Mrefa) kilifanikiwa kumaliza mvutano huo majira saa 10:04 alasiri na Simba kukubali kuketi benchi la kushoto. Kwa ujumla kulifanyika vituko vingi vyote vikiashiria imani za kishirikina, lakini kubwa zaidi ni baada ya kuridhia kukaa benchi la upande wa kushoto mmoja wa maofisa wa Simba alionekana akitoka kwenye basi lao akiwa na chupa mbili za maji ambayo hayakuwa na rangi ya kawaida, akaenda moja kwa moja kwenye benchi walilopaswa kulitumia na kuanza kuyamwaga.
Hali kama hii si mara ya kwanza kufanywa na timu kongwe za hapa nchini, jambo ambalo linatufanya kuzidi kuamini kwamba viongozi wa klabu hizi hawawezi kuisaidia TFF katika mchakato wake wa kukuza soka la Tanzania na badala yake wanazidi kulididimiza siku hadi siku.
Kuendelea kuamini ushirikina kunadhohofisha soka letu huku wajanja wachache wakinufaika kwa kuchota kiasi kikubwa cha fedha kwa madai ya kuzisaidia klabu kiushirikina. Tunakubali kuwapo kwa idara ya kamati za ufundi hata kwa klabu kubwa za nchi zilizopiga hatua kisoka, lakini kazi zao si za kushughulika na mambo ya kishirikina kama ilivyo hapa kwetu, kwani husimamia shughuli zote za kisaikolojia kwa wachezaji za kuandaa mazingira mazuri ya ushindi na kuepuka kuhujumiwa.
TFF bado ina kazi kubwa katika kuhakikisha inasimamia kwa kina na kupinga vitendo hivyo kwa kuongeza adhabu kali zaidi ikiwemo kuwapo kwa kipengele cha kuwafungia viongozi wa klabu kujishughulisha na soka endapo timu zao zitabainika kujihusisha na vitendo vya kishirikina.
Pasipo kufanya hivyo, soka la Tanzania litazidi kudidimia kwani viongozi wa klabu ambazo ndizo msingi mkubwa wa timu ya taifa wameonekana kuwekeza zaidi katika ushirikina badala ya kulea na kuendeleza vipaji.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment