Monday 13 April 2015

Shimbumbu wanavyobadili mawe ili kupata maji





Arusha.Katika karne ya 15 na 16 , kulikuwa na biashara ya ubadilishaji bidhaa kwa bidhaa. Watu wa jamii moja waliweza kupata mali na bidhaa walizohitaji kwa kubadilishana na jamii nyingine.
Biashara hiyo kwa namna moja au nyingine iliwaumiza watu wa upande mmoja na kuwatajirisha wa upande wa pili.
Mathalan, baadhi ya watu walibadilisha dhahabu kwa shanga au nguo, wengine wakabadili pembe za ndovu wakati mwingine kwa pipi na magobole.
Mambo hayo sasa yamebaki historia au simulizi ya mchana kwani uelewa na mazingira ya wakati huo yalijitosheleza kufanya hivyo hata bila ya kuhoji.
Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kuona hata katika karne ya 21, bado kuna maeneo ya Tanzania, ambayo watu wake wanafanya biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa maarufu ‘butter trade’ licha ya kutambua kuwa wanaumizwa lakini wanakosa njia mbadala wa kujikwamua.
Ndivyo ilivyo kwa wakazi wa Kijiji cha Shimbumbu, wilayani Arumeru linapokuja suala la maji. Kwao licha ya kuwa ni mahitaji ya msingi katika maisha, imekuwa bidhaa adimu na ya thamani kubwa inayoweza kufananishwa na dhahabu.
Kwa wakazi wa kijiji hicho, maji hugombaniwa na mwenye nguvu, ndiye atakayepata na wamefikia hatua ya kubadilishana mawe ya kujengea ili kupata bidhaa hiyo. Hilo linatokea sasa katika karne hii ya 21.
Licha ya kijiji hicho kuwa kilomita chache kutoka katikati ya Jiji la Arusha, ambalo lina utajiri wa madini ya Tanzanite na utalii, wakazi wake wana shida kubwa ya maji.
Kwa haraka, mazingira ya kijiji hicho yanaonyesha kuwapo uharibifu mkubwa wa mazingira na ukame yanayowaweka wakazi wake kwenye hali ngumu ya maisha, licha ya ardhi yenye rutuba waliyojaliwa.
Maisha ya Watanzania wa Shimbumbu yanaakisi yale ya enzi za ujima, huku ikionekana milima ya mawe yaliyochimbwa yakisubiri malori ya maji yafike ili baishara ya budalishana ifanyike.
Mamia ya ndoo na madumu yaliyo kando ya mawe yanasubiri ‘kuwa maji’ kwa kubadilishana hali ambayo wakati mwingine huwa kama sinema kutokana na kugombania.
Jambo hilo linaweza kutajwa kuwa ni aibu inayotokana na udhaifu wa kimkakati ikiacha maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu binadamu wa Shimbumbu kuishi katika ujima kwenye karne ya sasa.
Katikati ya kijiji hicho kuna mlima wenye mawe ambayo wananchi hujazana wakiyachimba wakiwa na ndoo za maji wakisubiri wateja.
Swali ni je, mawe yakiisha, wananchi hao wataishije, au utakuwa mwisho wa kunywa maji?
Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Arumeru, Happiness Mrisho anasema upembuzi ulishafanyika kwa muda mrefu na kiasi cha Sh120 milioni zinatakiwa kumaliza tatizo la maji kwa wakazi wa kijiji hicho.
Mbali na shida hiyo, barabara za eneo hilo zimeharibiwa kutokana na kubeba mizigo mizito bila ya kufanyiwa matengenezo na hazifai tena licha ya eneo hilo kuwa na watu wengi.
Diwani wa Kata ya Shimbumbu, Wilson Nyiti anasema kijiji hicho kina jumla ya wakazi 3,500 wanaotokana na kaya 750 na zote hazina maji.
Nyiti anasema adha hiyo imesababisha matatizo makubwa kwa wananchi, ikiwamo migogoro ya ndoa, hasa za utotoni.
Anasema mazingira ya kijiji hicho ni mabaya na hayafai, lakini hakuna jinsi ya kuwazuia wananchi kwani biashara hiyo ndiyo inayowapa mlo wao na familia kusoma.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana wakati wa ziara yake ya hivi karibuni aliliona hilo.
Katika ziara hiyo, Kinana anaonyesha mshangao na kueleza masikitiko yake kwa eneo hilo kutengwa.
“Hali hii siyo nzuri hata kidogo, barabara mbovu sijapata kuona, mazingira yameharibika kwa kiasi kikubwa tatizo la Sh120 milioni, ni aibu,” anasema Kinana.
Bila shaka wahusika wataliona tatizo hilo la wana Shimbumbu na kulifanyia kazi ili kunusuru milima na mazingira ikiwamo kuwapa nafasi kina mama kufanya shughuli nyingine. Lakini si kijiji hicho pekee kinachokabiliwa na shida ya maji, bali eneo kubwa la Mkoa wa Arusha na maeneo mengi nchini.
Machi 16, wananchi wa Arusha walifanya maandamano hadi ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (AWSA) wakidai kupata maji.
Maandamano hayo yaliyokuwa ya kushtukiza yalifanyika wakati maofisa wa AUWSA walipokuwa wakijadili kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji iliyohitimishwa Machi 21.
Tukio hilo lilisababisha Mwenyekiti wa Bodi ya mamlaka hiyo, Felix Mrema, Mkurugenzi wa AUWSA, Mhandisi Lucy Koye na wajumbe kukatisha mkutano wao na kukutana na wananchi walioandamana kwa lengo la kutoa ufafanuzi.
“Maji yaliyopo kwenye chanzo chetu hayatoshelezi mahitaji ya wananchi, mamlaka inatafuta vyanzo vingine,” alieleza Mhandisi, Koye.
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, aliyefika kwenye tukio hilo alieleza kuwa katika suala hilo hakuna siasa, bali amekwenda kuungana na wananchi ili kusaidia kutafuta ufumbuzi wa tatizo la maji akiwataka wananchi kuiwezesha AUWSA kuzalisha maji zaidi kwa kuondoa vikwazo vilivyopo.
Hata hivyo, takwimu za Serikali zilizotolewa katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe mkoani Mara mwezi uliopita zinaonyesha kuwa zaidi ya wananchi milioni saba wanapata majisafi na salama katika miji ya mikoa, wilaya na miji midogo nchini kutokana na kuboresha huduma za majisafi na uondoaji majitaka mijini.
Profesa Maghembe alisemas uboreshaji huo uliofanyika ni kujenga, kukarabati na kupanua miundombinu ya majisafi katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo na miradi ya maji ya kitaifa.
“Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imejenga miradi mipya 663 katika vijiji 10 kwa kila halmashauri nchini na miradi 68 ya upanuzi na ukarabati kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Utekelezaji huo umekamilisha miradi 731 iliyopangwa kutekelezwa na unajumuisha miradi 390 ambayo haikukamilika katika mwaka wa fedha 2013/2014,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema kuanzia Julai 2013 hadi Desemba 2014, jumla ya miradi 674 ya maji ilijengwa na kukamilika, idadi ambayo inachangiwa na ujenzi wa miradi mipya 433 ya vijiji 10 katika kila halmashauri na miradi mingine 241 ya upanuzi na ukarabati.
“Vijiji 900 vimepatiwa maji na jumla ya vituo 1,8610 vya kuchotea maji vimejengwa ambavyo vinahudumia watu 4,568,402 na kuanzisha vyombo vya watumia maji 560,” alisema na kuongeza.
“Usimamizi huo umeongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama vijijini kutoka asilimia 40 Julai 2013 hadi asilimia 53.08 za sasa.”

No comments:

Post a Comment