Tuesday 21 April 2015

Yanga kutangaza ubingwa Jumatatu

ashabiki wa Yanga wakishangilia kwa kuonesha mfano wa kombe
Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 24 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo 1965.
Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga huenda wakatangaza ubingwa  Jumatatu ijayo kama watashinda michezo yake mitatu wiki hii dhidi ya Stand United, Polisi Morogoro na Ruvu Shooting.
Mabingwa mara 24, Yanga baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Etoile du Sahel Jumamosi katika mchezo wa Kombe la Shirikisho,  wanahitaji ushindi dhidi ya Stand United leo kabla ya kuivaa Polisi Morogoro Ijumaa na kumalizia na Ruvu Shooting Jumatatu ijayo.
Yanga sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 46, kama itashinda mechi tatu hizo kati ya tano itafikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwani hata mabingwa watetezi Azam walio nafasi ya pili na pointi 42 kama itashinda michezo yake minne iliyobakia itafikisha pointi 54.
Pamoja na ratiba hiyo nyepesi kwa Yanga, kizingiti pekee kwao kwa sasa ni wimbi la majeruhi linaloiandama timu hiyo baada ya mabeki wawili wa kati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani kuikosa mechi ya leo dhidi ya Stand United  kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nahodha Haroub ‘Cannavaro na Yondani waliumia katika mchezo dhidi ya  Etoile du Sahel pamoja na  Salum Telela wote jana walishindwa kufanya mazoezi na wenzao.
 Daktari wa Yanga, Juma Sufiani aliliambia gazeti hili kuwa Cannavaro, Telela na Yondani hawatacheza mchezo wa leo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya vifundo vya miguu.
“Walikuwapo mazoezini ila hawakufanya na wenzao, Telela na Cannavaro tumewapeleka kufanyiwa vipimo na majibu yataletwa kesho (leo) ili tujue hali zao zinaendeleaje,” alisema Dk. Sufiani.
Kutokana na majeruhi hayo kocha wa Yanga, Hans Pluijm atalazimika kumtumia Mbuyu Twite na Rajab Zahiri kucheza beki ya kati katika mechi ya leo kuziba mapengo ya Yondani na Cannavaro, wakati  Said Makapu atacheza kama kiungo mkabaji akisaidiana na Hassan Dilunga na Haruna Niyonzima kuziba pengo la Telela.
Kocha Pluijm alisema wanasau kwa muda mambo ya Kombe la Shirikisho na wanaingia kwenye ligi kusaka ubingwa tu na watahakikisha wanapambana vilivyo ili kushinda michezo yote iliyobakia.
 “Sasa tuna mawazo ya ubingwa tu, tunajua kuwa mechi na Stand  United itakuwa ngumu kwani kila timu tunayokutana nayo imejiandaa, lakini tumedhamiria kupambana na kuhakikisha tunashinda michezo yetu mitatu mfululizo ili tuchukue ubingwa mapema,”alisema Pluijm.
Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal alisema wamejiandaa vizuri kuikabili Yanga huku akidai hawaihofii hata kidogo.
“Tunaichukulia Yanga kama timu ya kawaida, wachezaji ni wale wale, viwango vyao  havijabadilika, ila tu nikiri Yanga morali iko juu hivi sasa,” alisema Bilal.
Mshambuliaji tegemeo wa Stand United, Mnigeria Abaslim Chidiebele alisema alikuwa anaisubiri  Yanga kwa hamu ili kutimiza lengo lake la kuzifunga timu kongwe nchini.
Chidiebele alisema hajawahi kucheza kwenye Uwanja wa Taifa hivyo anataka kuweka historia kwa kuifunga Yanga kama alivyofanya dhidi ya Simba mjini Shinyanga.
“Hao mabeki ni majina tu lakini uwezo ni ule ule kama mabeki wengine, nitapambana mpaka nihakikishe nimefunga bao zaidi ya mbili nataka kufanya hivyo kwa kuwa ndio mara yangu ya kwanza kucheza ndani ya nyasi za Uwanja wa Taifa,”alisema Chidiebele ambaye amefunga mabao tisa msimu huu.

No comments:

Post a Comment