Sunday 26 April 2015

Takrima: CCM katika hatari uchaguzi 2015.

Takriban wanachama 21 wanatajwa kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake wa vipindi viwili vya miaka mitano vinavyoruhusiwa kikatiba, na makada sita wanaonekana kuwa na nguvu zaidi wanatumikia adhabu ya kutogombea uongozi baada ya kubainika kuanza kampeni mapema..

Zanzibar. Mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar Hassan Mussa Takrima (72) ameionya CCM kuwa itakuwa katika hatari ya kushindwa vibaya kwenye Uchaguzi Mkuu kama kitasimamisha “mgombea mwepesi, asiye na mvuto na asiyekubalika kwa wananchi”.
Takriban wanachama 21 wanatajwa kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake wa vipindi viwili vya miaka mitano vinavyoruhusiwa kikatiba, na makada sita wanaonekana kuwa na nguvu zaidi wanatumikia adhabu ya kutogombea uongozi baada ya kubainika kuanza kampeni mapema.
Wakati CCM ikitafakari jinsi ya kupata mgombea wake, vyama vinne vya upinzani na vyenye nguvu zaidi, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa urais na pia katika ngazi za ubunge na udiwani.
Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake Kijiji cha Jumbi kuzungumzia miaka 51 ya Muungano, Takrima, , ambaye aliwahi kuwa naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, alisema kutokana na mabadiliko ya  hali ya kisiasa yanayoendelea kujitokeza nchini, CCM inatakiwa kuchagua mgombea imara kama jiwe kwa kuangalia sifa na uwezo wa kukabiliana na vuguvugu la upinzani kutoka na mazingira ya  ya kisiasa yanayoendelea kujitokeza Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kwamba ni jambo la kushangaza wakati imebakiwa miezi sita ya kufanyika uchaguzi mkuu, hadi sasa CCM imeshindwa kuweka hadharani mgombea wake wa urais wa Muungano, Zanzibar na nafasi nyingine ili wananchi wapate muda wa kutosha kuwachambua sifa uwezo na uadilifu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu.
Alisema yapo mataifa wagombea wa nafasi nyeti kama hiyo ambayo hujulikana mwaka mmoja kabla ya ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ili kuwapa nafasi  wananchi ya kuwachambua pamoja na kuziba nyufa za kisiasa kama zitatokea wakati wa mchakato wa kupatata mgombea.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula alisema juzi kuwa utaratibu huo katika mazingira ya Tanzania unaweza kuzua malumbano na migongano kwa kuwa baadhi ya wnasiasa wanatumia fedha zaidi.
Aidha alisema kwamba iwapo CCM itakaribisha mizengwe katika kupata mgombea wa urais wa Muungano katika vikao vyake, inaweza kuandika historia mpya ya kisiasa na kutaka haki na usawa kutumika.
Alieleza kwamba Watanzania bado wana imani kubwa na CCM pamoja na kasoro mbalimbali zinazojitokeza yakiwemo matatizo ya ufisadi baada ya kufanikisha kazi kubwa ya kuimarisha amani na umoja wa kitaifa.
Alieleza kwamba  uwezi kujenga nyumba imara bila ya kuwa na mawe, chokaa na maji na kusisitiza kuwa lazima CCM isimamishe  mtu mwenye msingi wake binafsi wa kisiasa mvuto kwa wapinga kura pamoja na kuwa mtu anayekubalika kutokana na usafi wake.
Hadi sasa viongozi wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi maalum Professa Mark Mwandosya, Waziri wa Kilimo na Ushirika Stiven Wasira na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe
Wengine ni Professa Anna Tibaijuka, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari  Makamba, mbunge wa Sengerema Wiliam Ngeleja, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na balozi Mstaafu Ali Abeid Karume. Kuhusu mikasa ya ufisadi nchini alisema hali inaendelea kuwa mbaya kutokana na serikali kutowachukulia hatua vigogo wanaofanya vitendo hivyo na kueleza kuwa kashifa ya kununuliwa mabehewa machakavu ya treni inatisha na kusikitisha kutokana na sekta ya usafirishaji kuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi katika kukabiliana na matatizo ya umasikini.

Alisema kwamba vitendo vya ufisadi  vimekuwa kama fasheni kutokana na vigogo wanaofanya vitendo hivyo wakiwemo watendaji kuendelea kulindwa na Serikali licha ya kuwa wanahujumu uchumi wa nchi.
Akizungumzia hali ya kisiasa ya visiwani hapa, Takrima alisema Serikali ya Ummoja wa Kitaifa (SUK) imesaidia kuimarisha misingi ya amani na umoja wa kitaifa baada ya wananchi kuishi kwa muda mrefu wakitengana na kususia shughuli za kijamii kama maziko na harusi kwa sababu za kisiasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Hata hivyo alisema kwamba kumeanza kujitokeza cheche zinazohatarisha amani na mshikamano.

No comments:

Post a Comment