Tuesday 14 April 2015

Uandikishaji ukamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu

 
Serikali hii inashangaza. Mwishoni mwa mwaka jana ilipotangaza kwamba Aprili 30 mwaka huu itakuwa siku ya kupiga Kura ya Maoni kwa Katiba Inayopendekezwa iliona mbali sana.
Serikali ilielezea ilivyojipanga kuhakikisha Kura ya Maoni inafanyika kwa ufanisi; kwamba asasi za kutoa elimu zitaruhusiwa kufanya kazi hiyo na timu za kampeni za NDIYO na HAPANA pia zingekuwa na muda wa kutosha.
Kwa kuzingatia muda, asasi za kiraia, vyama vya upinzani na wasomi walionyesha shaka yao juu ya tarehe hiyo kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) isingeweza kukamilisha uandikishaji mapema na kusimamia kura hiyo.
NEC ilisita kuwajibu wenye shaka na ilisita kujifunga kuwa inaweza hadi ilipoahidiwa kupewa mashine za BVR 8,000 kati ya 15,000 ilizoomba kwa ajili ya kuandikisha wapigakura. Hapo ikawa inasisitiza kuwa itakamilisha kazi hiyo mapema hivyo Kura ya Maoni itakuwepo kama ilivyopangwa.
Hivi sasa, kila mmoja ni shahidi kwamba mwaka 2014 uliisha bila mashine hizo kuwasili. Kila mmoja ni shahidi pia kwamba ilipofika Januari hadithi ikawa mashine ziko njiani na hata NEC ilipoanza kuandikisha wapigakura Februari 23 kwa kutumia BVR 250 ilizokuwa nazo, katika Mkoa wa Njombe, haikupewa mashine za ziada.
Kuona hivyo, NEC, bila aibu,ilikwenda Nigeria na Kenya kuomba mashine za BVR lakini ilinyimwa. Nigeria walikataa kwa vile nao walikuwa wanakabiliwa na uchaguzi mkuu Machi 28 huku Kenya wakisema wanatumia kuboresha daftari lao kila siku.
Aprili 2, NEC ikiwa imeelemewa na mzigo wa lawama na shutuma, ililazimika kutangaza kuahirishwa kwa Kura ya Maoni hadi hapo itakapotangazwa tena. Mpaka sasa NEC haijakamilisha uandikishaji wapigakura Njombe. Je, itamaliza lini nchi nzima kwa ajili ya uchaguzi mkuu?
Kwa ratiba ya matukio ya mwaka huu – vikao vya uteuzi wagombea urais, ubunge na udiwani, Bunge la Bajeti, kampeni za uchaguzi mkuu – hatuoni uwezekano wa kufanyika mwaka huu, labda itokee miujiza.
Hofu yetu kubwa ni kwamba kusuausua uandikishwaji wapigakura kulikosababisha Kura ya Maoni kuahirishwa ndiko tunaona kunajirudia kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 30 mwaka huu.
Serikali inaona ni mbali sana, NEC inaona mbali sana, chama tawala, CCM, kinaona mbali sana na wafuasi wa chama hicho wanaona mbali sana.
Je, si kweli kwamba Serikali iliona tarehe ya Kura ya Maoni iko mbali sana? Je, viongozi wa CCM na NEC si waliona Aprili 30 iko mbali sana? Hadi leo mashine za BVR hazijaongezeka, uandikishaji tena katika mkoa huo mmoja unakwenda mwendo wa konokono na kuna hatari tukafika Oktoba watu wengi wakawa hawajapata nafasi ya kuandikishwa.
Tunaamini kusuasua huku si bure. Serikali inajua kila baada ya miaka mitano unafanyika uchaguzi mkuu mwingine, kwa nini imesubiri hadi dakika za mwisho ndipo inahamanika kutafuta BVR?
Vilevile, Serikali ndiyo ilitangaza mwaka 2012 kwamba uandikishaji utakuwa kwa mfumo wa BVR, kwa nini ilisubiri dakika za mwisho ndipo ianze kukimbia huku na kule kwenda kuazima kutoka nchi jirani badala ya kununua?
Serikali itafute fedha haraka inunue mashine na kazi ya uandikishaji ifanyike kama ilivyopangwa ili wananchi watumie haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka. Hatutapenda kusikia visingizio vyovyote vikitumika kuathiri uchaguzi mkuu.

No comments:

Post a Comment