Monday 13 April 2015

MCHAKATO WA KATIBA MPYA: Miezi mitano ya sintofahamu kuhusu BVR, Kura ya Maoni



Baadhi ya wananchi wakishiriki upigaji kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana   . Picha ya Maktaba 




Ilichukua miezi mitano kumaliza mvutano wa kimahesabu na maneno baina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Serikali na wadau wa demokrasia kuhusu muda wa maandalizi na upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Kwa miezi hiyo yote tangu Rais Jakaya Kikwete alivyotangaza Oktoba, 2014 kuwa kura hiyo ingefanyika Aprili 30 mwaka huu, vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wananchi walipinga na kuomba iahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu.
Mbali na hoja ya kutaka shughuli hiyo ifanywe bila presha, bado kusuasua kwa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR), kulizidi kuonyesha hesabu za wazi kwamba isingewezekana.
Hata hivyo, Serikali na Nec walisisitiza tarehe hiyo inayodaiwa kutangazwa na Rais Kikwete kinyume na Sheria ya Kura ya Maoni 2014. Uamuzi wa Nec kuahirisha zoezi hilo hadi litakapotangazwa tena kwa mashauriano na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, umeleta ushindi kwa wakosoaji hao.
Uhuru wa Nec shakani
Asilimia kubwa ya wakosoaji wanasema kuwa kitendo cha Nec kung’ang’ania kisichowezekana ni uthibitisho haina uhuru. Uhuru huo, kwa mujibu wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda, ulijidhihirisha baada ya tume hiyo kushindwa kujiendesha katika uamuzi na mipango.
“Kuahirishwa kwa Kura ya Maoni ni kitu kilichotarajiwa kwa sababu tarehe iliyopangwa isingeweza kufikiwa kirahisi na aliyeitangaza haikuwa Nec.
“Hii inatufunza taasisi lukuki za umma hazijiendeshi kiweledi. Zilitakiwa kujiendesha kwa taratibu na kuwajibika ili kila tamko litekelezeke na siyo kubadili kama ilivyotokea,” anasema Mbunda.
Hoja ya Uhuru wa Nec isingevuma iwapo ingenyooshea mikono zoezi hilo mapema kutokana na kusuasua kwa uandikishaji kwa BVR.
 Licha ya kujua kuwa muda huo usingewezekana, Nec iliendelea kuubeba mzigo huo mzito ambao mara kwa mara Jaji Lubuva alikuwa akisisitiza yeye ni ‘Mnyamwezi’ mbebaji wa mzigo mzito na kwamba iwapo ungemshinda angesema kama alivyofanya Aprili, 2.
Wadau wamemlalamikia Rais Kikwete kwa kuvunja Sheria ya Kura ya Maoni kwa kutangaza tarehe badala ya muda kama sheria inavyomtaka na kuwaachia kibarua kizito Nec kukabiliana na kisichowezekana.
Mwanasheria Halord Sungusia anasema kitendo cha kuahirisha tarehe ya Kura ya Maoni, kinadhihirisha nguvu ya kisheria ya Nec juu ya tukio hilo la mwisho la Katiba Mpya.
“Nec imefanya jambo zuri kwa sababu hayo ndiyo mamlaka iliyopatiwa kisheria. Kwa bahati mbaya yalipokwa na Rais. Kifungu cha tano cha Sheria ya Kura ya Maoni kinaipa Nec nguvu ya kutangaza tarehe mahususi ya kura wakati Rais anatakiwa tu kutangaza muda,” anasema Sungusia.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, Rais hakuwa amevunja sheria yoyote na kwamba alifanya hivyo “in the Spirit of law” (ndani ya dhamira ya sheria) kwa kuwa kifungu namba nne cha sheria hiyo kinampa madaraka hayo japo tarehe ya kutangaza ni yao.
Jaji Lubuva katika mkutano wake na Waandishi wa Habari hivi karibuni alisema tume yake ipo huru kama ilivyoanzishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya 1977 na kwamba yeye, Makamishna au Wakurugenzi wake hawajawahi kuingiliwa kiutendaji.
“Kumekuwa na dhana kuwa tume yetu haipo huru kwa sababu viongozi wanateuliwa na Rais na sisi kwenye Katiba Mpya tulipendekeza mabadiliko. Sasa tukiacha shughuli kwa sababu ya dhana hiyo, mambo hayataenda. Ila ikitokea imeamuliwa waje wengine sisi tutaondoka,” anasema Jaji Lubuva.
Kuahirishwa kwa Kura ya Maoni ni matokeo ya mwenendo mbovu wa uandikishaji wapigakura kwa BVR ambao umegubikwa na ukata wa kibajeti.
Nec ilijikuta katika wakati mgumu tangu awali baada ya idadi ya mashine walizokuwa wakihitaji kuendelea kupunguzwa kutoka 15,000 hadi 10,500 na baadaye idadi ya sasa mashine 8,000.
CCM inahusika na yaliyotokea
“Tume inaonekana wazi kuwa haikuwa huru. Ilisema kabisa haina vifaa vya kutosha lakini iliendelea kulazimisha kuwa Kura ya Maoni ingefanyikakwa tarehe iliyopangwa. “Hata mtu ambaye hajasoma hesabu alikuwa anajua kuwa isingewekana kura hiyo kupigwa Aprili, 30,” anasema Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Isaiah Salmon. Anasema tamko la Rais Kikwete juu ya tarehe hiyo lililenga kuwapumbaza wananchi ili CCM ijiandae na Uchaguzi Mkuu na ulazimishaji huo ulifanywa kwa makusudi kwa masilahi ya kisiasa.
 ‘Ujanjaujanja huo, anasema utaathiri imani ya wananchi kwa Rais Kikwete na serikali yake kuwa huenda kuna mambo mengi hufanywa kwa presha,” anasema Salmon.
Iwapo kulazimishwa kwa Kura ya Maoni kulifanywa kwa masilahi ya CCM na Serikali inakosa uhakika kutokana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema chama chake hakihusiki na ‘uzembe’ huo.
“CCM hatuhusiki na haihitaji kwenda shule kujua kuwa tangu awali mambo hayakuwa mazuri. Kimsingi hawa watu (Nec) lazima wawajibike…ikifikia mahala umeshindwa, wajibika.“Lazima tuseme wazi hii ni nyeupe na hii ni nyeusi,” anasema Nape.Nape anaenda mbali na kuwatuhumu viongozi wa Nec kwamba walipanga ‘kupiga pesa’ kwa vikao na semina” huku akimtetea Rais Kikwete kwa kusema “siamini kama Rais alitangaza bila kupata ushauri wa tume. Naamini kulikuwa na mawasiliano baina yao.

No comments:

Post a Comment