Tuesday 14 April 2015

Wenye ulemavu watengewa mamilioni ya uchaguzi mkuu



Dar es Salaam. Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya The Foundation for Civil Society (FCS), imetenga Sh 300 milioni kwa ajili ya kugharamia elimu ya uchaguzi mkuu kwa watu wenye ulemavu.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga aliliambia gazeti hili jana kuwa fedha hizo zitagawiwa kwa asasi za watu wenye ulemavu zilizosajiliwa tu.
“ Ushiriki wa watu wenye ulemavu katika michakato ya kidemokrasia mara nyingi umekuwa hafifu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo hali yao ambayo baadhi huwawia vigumu kufika hata kwenye vituo vya kupigia kura,” alisema Kiwanga.
Alisema, pia kuna tatizo la upatikanaji wa taarifa za msingi zinazohusu mchakato wa Kura ya Maoni na uchaguzi. Hii inatokana na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya kundi hilo la watu wenye ulemavu, alisema.
Hii si mara ya kwanza
Alisema kuwa hii ni mara ya pili taasisi hiyo kutoa fedha za kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu. Awali tulifanya hivyo wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2010, alisema. Alifafanua kuwa ruzuku ya 2010, ilitolewa baada ya asasi hizo kubainisha changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu kuelekea kwenye uchaguzi huo.
“FCS tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na watu wenye ulemavu na sasa tunaamini hatua hiyo ya kuwasaidia katika upatikanaji wa elimu, itawawezesha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo unaopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema.
Kiwanga alitaja baadhi ya matatizo yanayowakabili watu wenye ulemavu nyakati za chaguzi kuwa ni pamoja na kukosekana kwa watafsiri wa lugha za alama wakati wa kampeni na hata katika vituo vya kupigia kura.
Alieleza kuwa taasisi hizo za kiraia bara na visiwani, zinatakiwa kutuma maombi ili kupata fedha hizo zinazotolewa kama ruzuku kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Watu wenye ulemavu wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, hivyo tunatoa ruzuku hiyo ili kuziwezesha asasi zao kuendesha mafunzo na kuwashawishi watu wenye uwezo wajitokeze, watambue haki yao ya kikatiba na kugombea nafasi mbalimbali.
Pia tunawataka wadau kuandaa mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki uchaguzi huo kikamilifu.,” alisema.
Alisema FCS inatoa ruzuku hiyo kama sehemu ya wajibu wake katika kuhakikisha kuwa jamii ya watu wenye ulemavu nayo inashiriki uchaguzi mkuu katika hatua zote; kujiandikisha kwenye Daftari la Kuduma la wapigakura, kugombea, kuchagua na kuchaguliwukumu lake la kuhakikisha kwamba asasi za kiraia zinakuwa chachu kwenye mchakato wa maendeleo, wenye kulenga kuleta mabadiliko kwa wananchi na kuwawezesha kutambua utekelezaji wa sera, utawala bora na uwajibikaji.

No comments:

Post a Comment