Na Rhoda Simba
Waziri wa Maji na Umwagiliaji
Mhandisi Gerson Lwenge ametaka watendaji wa Halmashauri nchini
kuwashtaki watu wanaohujumu miundombinu ya maji kama wahujumu uchumi.
Hayo aliyasema leo alipofanya
ziara katika kijiji cha Bumila kata ya Lupeta Halmashauri ya Mpwapwa
baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya maji katika kijiji hicho.
“Naagiza Halmashauri muwatafute
watu wote waliohujumu miundombinu ya maji na washitakiwe kama wahujumu
uchumi, hatuwezi kuwaachia watu wanaosababisha wananchi wasio na hatia
kukosa huduma muhimu ya maji”
Miundombinu ya maji katika kijiji
cha Bumila imehujumiwa kwa mabomba zaidi ya 40 ya nchi 2 yenye urefu wa
mita 6 kwa kila kipande cha bomba kung’olewa na hatimaye maji
kutokuwafikia wananchi.
Katika hali ya kulikabili tatizo
la maji katika kijiji hicho Mhandisi Lwenge ameiagiza Halmashauri ya
Mpwapwa kuchimba kisima katika kijiji cha Bumila haraka ili kuwaondolea
adha wananchi wa kijiji hicho.
Katika hatua nyingine Waziri
Lwenge amewataka viongozi na watendaji wote nchini kushughulikia maswala
ya maji badala ya kuachiwa yeye Waziri wa Maji peke yake.
“Kila mmoja wetu kwa nafasi yake
ana jukumu la kufatilia maswala haya sio ya waziri wa maji peke yake,
Wilayani mkishindwa mpeleke Mkoani nao wakishindwa wataleta Wizarani
nasi tukishindwa tutapeleka kwa Magufuli kitu ambacho sitegemei” Alisema
Waziri Lwenge.
Akiwa Wilayani Chemba, Waziri
Lwenge amekataza tabia ya baadhi ya vijiji, kata na jamii za watu wanao
wabagua jamii nyingine katika miradi ya maji. Akiwa wilayani humo Lwenge
aliagiza kuwa miradi yote ya maji ni mali ya serikali hivyo jamii zote
bila kujali mipaka ya kijiografia kupata huduma hiyo.
“Maji yote ni mali ya serikali,
hamna mtu wala kikundi cha mtu chenye kumiliki maji, hivyo hairuhusiwi
kwa mtu au kikundi cha watu kujimilikisha maji na kubagua baadhi ya
jamii ya watu wengine wasipate maj, sisi sote ni watanzania”. Alisema
Waziri Lwenge.
Ziara ya Waziri Lwenge ilianza
katika Halmashauri za Chemba na Kondoa na kuishia katika halmashauri ya
Mpwapwa ikiwa ni ahadi aliyoitoa bungeni kwa mbunge wa Chemba Juma
Nkamia na Mpwapwa George Lubeleje.
No comments:
Post a Comment