Thursday 23 June 2016

Jeshi la Polisi linazindua mpango wa kuboresha usalama katika jamii

 
Jeshi la Polisi nchini, linatarajia kufanya  uzinduzi wa mpango wa kuboresha usalama wa jamii na mali zao, ambao una dhamira ya kupunguza uhalifu nchini. Mpango huu utaanza kutekelezwa katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni kuanzia mwezi wa Julai mwaka huu na baadaye kuufikisha katika mikoa yote nchini mwanzoni mwa mwaka 2017.
 
Uzinduzi huo utafanyika  siku ya Jumamosi, tarehe 25 Juni, 2016 katika viwanja vya Biafra, Kinondoni Dar es Salaam, kuanzia saa tatu asubuhi, ambapo Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe. Dr John Joseph Pombe Magufuli. Sambamba na uzinduzi huo wa mpango, Mhe. Rais ataanza kuzindua kituo cha Mawasiliano ya simu za dharura za Polisi 111, na 112 (Police Call Centre) na kituo cha Polisi cha kuhamishika kilichopo maeneo ya Coco beach mkabala na jengo la Coco Plaza, ambacho ni miongoni mwa vituo 13 vitakavyowekwa kwenye maeneo tete kiuhalifu yaliyoainishwa katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.

Lengo la Mpango huu ni kuimarisha usalama wa wananchi katika jamii na mali zao. Huu ni ubunifu wa Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake ambapo Jeshi la Polisi limeamua kuondokana na utendaji wa kimazoea  kwa kuanzisha mikakati mikuu minne ambayo ni  kuongeza ufanisi katika shughuli za kipolisi, kuongeza ubora katika utoaji wa huduma za kipolisi, kuimarisha mawasiliano na ushiriki wa wadau pamoja na kubuni  vyanzo mbalimbali katika kutafuta rasilimali fedha. 

Kupitia mikakati hiyo, Jeshi la Polisi litaanzisha mpangilio mpya wa ulinzi na doria katika  maeneo yaliyokithiri kwa uhalifu, litaboresha Vituo vya Polisi kuwa katika muonekano bora na wa aina moja nchi nzima, litaimarisha ubia na sekta binafsi za ulinzi, litaongeza uharaka wa kufika kwenye matukio ya uhalifu yanayoripotiwa, litaimarisha na kudumisha misingi ya maadili, litaweka mifumo thabiti ya kusimamia rasilimali watu, litaimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya Jeshi, na mwisho litatafuta vyanzo mbadala vya fedha zinazohitajika ili kuliwezesha Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wake. Vyanzo mbadala vitaongeza wigo wa kutafuta rasilimali fedha kutokana na ufinyu wa Bajeti ya Serikali ambayo Jeshi la Polisi limekuwa likipata kila mwaka.
Aidha, uzinduzi huo utasindikizwa na Wasanii mbalimbali wa Muziki wakiwemo, Bendi ya Polisi, ya Moto Band, Manfongo, Ndolela, Man Prince pamoja na wasanii wengine na burudani mbalimbali zitakuwepo.

Wananchi  wote  kwa ujumla wanakaribishwa ili kupata maelezo ya kina na uelewa juu ya mkakati huu mpya wa kimageuzi ulioandaliwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery Bureau-PDB) inayoratibu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Asanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,

No comments:

Post a Comment