Monday 27 June 2016

Baadhi ya mashabiki wanachama wa klabu ya Simba wamejitokeza makao makuu ya klabu ya Yanga na kuwataka Wanasimba kujitokeza kwa wingi na kuiunga mkono Yanga, kesho.

Baadhi ya mashabiki waliosema ni wanachama wa klabu ya Simba, wamejitokeza kwenye mkutano wa waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu ya Yanga na kuwataka Wanasimba kujitokeza kwa wingi na kuiunga mkono Yanga, kesho.
Yanga inashuka dimbani kuivaa TP Mazembe katika mechi ya Kombe la Shirikisho hatua ya Makundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Amaniel Mngonja na Rifat Maulanga wamejitokeza kwenye mkutano huo ulioongozwa na Msemaji wa Yanga, Jerry Muro katika makao makuu ya Yanga, Kaunda na Twiga jijini Dar es Salaam.

“Sisi sote ni mashabiki na wanachama wa Simba, tunawaomba mashabiki na wanachama wenzetu wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono Yanga.

“Yanga ndiyo inayoiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo, hivyo waje kwa wingi kuishangilia,” alisema Maulanga.

Kwa upande wake, Muro alisema kwa shabiki ambaye hataweza kuvaa jezi za Yanga, angalau avae jezi za Taifa Stars.


“Kama utashindwa basi vaa jezi ya Taifa Stars, lakini bado unaweza kuvaa jezi ya timu yako hata kama ni Simba lakini beba bendera ya taifa, tuishangilie Yanga ni kwa ajili ya Tanzania.”

Kuhusiana na uanachama wa Simba wa Maulanga na Mngonja, wote walikataa kutaja kadi zao za uanachama na kusisitiza hawakuwanazo hapo.

No comments:

Post a Comment