Mtendaji Mkuu TEMESA Dr. Mussa
Mgwatu (wa pili kushoto) akisikiliza Kaimu Meneja wa TEMESA Kagera Bw.
Wilson Nyitwa(wa pili kulia) alipotembelea ofisi hiyo na kuzungumza na
baadhi ya watumishi wa TEMESA Kagera kushoto ni Msaidizi wa Meneja wa
TEMESA Kagera Bw. Charles Mbegete na kulia ni Mhasibu Bi. Joviness
Samson.
Mtendaji Mkuu TEMESA Dr. Mussa
Mgwatu (katikati) akikagua chumba maalumu kwa ajili ya injini (Engine
Room) kulia ni msaidizi wa Meneja Bw. Charles Mbegete na kushoto ni
Kaimu Meneja TEMESA Kagera Bw. Wilson Nyitwa.
Mtendaji Mkuu TEMESA Dr. Mussa
Mgwatu (wa tatu kushoto) akiongea na baadhi ya watumishi wa TEMESA
Kagera alipotembelea kituoni hapo kukagua jinsi Ofisi inavyofanya kazi
na kuzungumza na wafanyakazi.
Picha Na Theresia Mwami TEMESA (Kagera).
Na Theresia Mwami TEMESA Kagera
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu amewataka watumishi wake kuacha
kufanya kazi kwa uzembe na mazoea badala yake waongeze ubunifu katika
miundombinu iliyopo ili kuweza kuzalisha zaidi ikiwa ni sanjali na
kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya madeni siku hadi siku.
Ameota agizo hilo alipotembelea
na kujionea hali ya karakana ya TEMESA mkoani Kagera na kumuagiza Kaimu
Meneja wa TEMESA Kagera Bw.Wilson Nyitwa kusimamia kwa makini
utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo mkoani hapo.
“Inatupasa kuanza na hiki kidogo
tulicho nacho kwa kuziba mianya ya uzembe na muongeze uadilifu na
ufuatiliaji katika kazi tulizo nazo tufanikishe utendaji wa kazi zetu”
alisema Dkt. Mgwatu.
Dkt Mussa Mgwatu ameongeza kuwa
watendaji wanapaswa kupambana ili kulinda soko lililopo kwa sasa na hata
kuongeza wateja zaidi. Kwa sasa wateja wa TEMESA ni taasisi za serikali
ambazo zinapeleka magari na mitambo kutengenezwa katika karakana zao.
Aidha kwa upande wake Kaimu
Meneja wa TEMESA Kagera Bw.Wilson Nyitwa alieleza kuwa Kituo chake
mbali na kuwa na karakana na kutengeneza magari na vifaa vya
umeme,kukodishaji mitambo na usimikaji umeme katika majengo mbali mbali
ya serikali pia kinasimamia uendeshaji wa vivuko viwili vilivyopo
Kyanyabasa na Ruvuvu.
Alieleza kuwa TEMESA Kagera ina
changamoto nyingi zikiwemo uchakavu wa Karakana yake iliyojengwa tangu
mwaka 1958 pamoja na kukosa vitendea kazi muhimu pamoja na magari kwa
ajili ya matumizi ya ofisi lakini bado wanafanya kazi kwa kujituma na
kuzalisha zaidi ya Shillingi Million 50 kwa mwezi.
“Nakuomba Mtendaji Mkuu
utusaidie gari moja kwa ajili ya matumizi ya kituo nyongeza ya mafundi,
vitendea kazi vya kisasa vya karakana ,ukarabati wa karakana ya mkoa ili
kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu na kuzalisha zaidi.
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt.
Mussa Mgwatu yupo katika ziara ya kikazi Kanda ya Ziwa na atatembelea
vituo vya TEMESA vilivyopo ili kubaini changamoto na kujionea utendaji
kazi wa vituo hivyo na kwa kuanzia yupo Mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment