Monday 31 October 2016

Wahariri waukubali Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari

nap7
Anitha Jonas – MAELEZO
Wahariri wa vyombo vya habari wameukubali Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari baada ya kuusoma kwa umakini nakuona namna gani utasaidia kuinua tasnia ya habari nchini.
Hayo yamebainishwa katika mahojiano maalum  kwa njia ya simu na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari akiwemo Mhariri wa Televisheni ya TV 1, Bw.Said Mwishehe huku akieleza faida za Muswada huo pamoja na kutoa maoni yake kwa kuiomba serikali kuangalia vizuri baadhi ya vipengele na kama kipengele cha 54 na 55 katika Sehemu ya Nane ili kuvipunguzia makali na kuondoa suala la kuonekana kubana uhuru wa vyombo vya habari.
“Kuna umuhimu kwa wadau wa habari kuunga mkono muswada huu badala ya kuupinga kwani una mambo mazuri yatakayosaidia kuboresha tasnia hii ya habari na kuipa heshima kama taaluma nyingine badala ya kuonekana kuwa waandishi wa habari ni watu wababaishaji tu na wasiyo na taaluma iliyo imara,”alisema Bw.Mwishehe.
Pamoja na hayo Mhariri huyo aliendelea kusema amefurahishwa na muswada kwa namna unavyojali maslahi ya waandishi wa habari pale unapoeleza kuwa wamiliki wa vyombo vya habari watahitajika kuwakatia bima waandishi wa habari  kwa hiyo itakuwa jambo la busara kwani waandishi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu yanayohatarisha afya zao pasipo kuwa na bima inayomlinda akiwa kazini.
Aidha, Bw.Mwishehe aliwasihi wadau wa sekta ya habari kutuma maoni yao kwa vile vipengele vya muswada vinavyoonyesha kutokuwa sawa na pia ameiomba serikali kuwa na utayari wa kuyapokea maoni hayo  kwa ajjili ya kuboresha muswada huo na kuufanya bora na wenye tija katika tasnia ya habari nchini.
Naye Mhariri wa Gazeti la Mtanzania, Bw.Revocatus Makaranga alisema Muswada huo wa habari una mambo mazuri yanayoipeleka tasnia mahali pazuri ikiwemo suala la waandishi wa habari kuhitajika kujiendeleza katika elimu ya juu  na hii itasaidia kukuza upeo wa mwandishi na kumfanya awe na uwezo mkubwa na kufanya kazi kwa kujiamini kama ilivyo kwa waandishi wa nchi zilizoendelea.
Bw.Makaranga aliongeza kusema muswada una vipengele ambavyo ipo haja ya serikali kuvifanyia marekebisho ikiwemo suala la adhabu inayotolewa kwa waandishi ya kuwafungia pale wanapokuwa wamekosea.
Pia mhariri huyo ameipongeza serikali kwa muswada huo ambao utaleta picha mpya ya kimaendeleo katika tasnia ya habari ikiwemo suala la  kuanzishwa kwa Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari nchini ambapo utasaidia kutoa elimu kwa waandishi mara kwa mara na kuwajengea uwezo wa utendaji.
Kwa upande wake, Mhariri Mkuu wa kituo cha Redio Efm, Bi Scolastika Mazula alisema katika muswada huo wa habari yapo mambo mazuri yenye tija katika sekta ya habari kama suala la kuanzishwa kwa Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari ni jambo jema sana kwani utasaidia kutoa fursa za waandishi kujiendeleza kimasomo na kuifanya fani ya habari kuwa na wasomi zaidi tofauti na inavyoonekana kwa sasa.
“Suala la elimu kwa waandishi ni bora liwekwe wazi kisheria kwani tansnia hii ya habari inahitajika kuheshimika kama ilivyo tansia nyingine badala ya kuonekana wababaishaji”, alisema Mazula.
Pamoja na hayo Bi. Mazula aliendelea kutoa maoni yake kuhusu Muswada kwa kusema kuwa  suala la kuanzishwa kwa bodi ni zuri ila ingekuwa vyema kama bodi hiyo itakuwa na asilimia kubwa ya wadau wa habari na ijitegemee na Waziri mwenye dhamana ya habari na Mwanasheria Mkuu wasiwe na mamlaka sana katika bodi hiyo.
Pamoja na hayo naye Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Bw.Neville Meena alisema kwa sasa wanajukwaa wameshatoa maoni yao kuhusu muswada huo na watayawasilisha kwa ajili ya kusaidia kuboresha muswada huo na kuufanya uwe na tija na manufaa zaidi katika kuendeleza tasnia ya habari nchini.

No comments:

Post a Comment