Thursday 27 October 2016

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, amewataka maafisa utumishi kuwapa nafasi baadhi ya wafanyakazi wanaoomba kwenda kujiendeleza kitaaluma

zili
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza baraza la  wafanyakazi mkoani humo katika kipindi cha mwaka 2016/2019(picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, amewataka maafisa utumishi kuwapa  nafasi baadhi ya wafanyakazi wanaoomba kwenda kujiendeleza kitaaluma badala ya kuwabania na kusababisha kudumaa kielimu.
Aidha ametoa rai kwa watumishi wa umma mkoani humo kuwajibika kwenye maeneo yao ya kazi pamoja na kuwatumikia wananchi kikamilifu.
Mbali na hayo mkuu huyo wa mkoa ,amesisitiza viongozi mbalimbali kwenye maeneo ya kazi  kujenga ushirikiano  wa kutosha na watumishi ili kuondoa malalamiko ambayo huwa yakijitokeza .
Mhandisi Ndikilo aliyasema hayo ,wakati akifungua baraza la wafanyakazi  mkoani Pwani mwaka 2016-2019 pamoja na kuchagua katibu  na katibu  msaidizi wa baraza hilo.
Hata hivyo alisema ni lazima kukubaliana na mabadiliko na kwenda na wakati kwa kukuza taaluma za watumishi  ili kuongeza uwezo kwenye maeneo yao ya kazi .
“Kiukweli tuliyojifunza darasani isiwe mwisho badala yake tuongeze elimu zetu kwa lengo la  kupanua elimu zetu ambazo wengi wetu tumezipata miaka mingi  iliyopita” alisema.
Mhandisi Ndikilo, alieleza kuwa ifikie wakati wa kujitambua na kuthamini nafasi walizonazo na kutamani kufika kwenye hatua nzuri ya kielimu.
Akizungumzia  suala la  uwajibikaji aliwaomba maafisa utumishi na makatibu tawala  wilaya na mkoa waendelee kuwa wawakilishi wakubwa  wa kuwasilisha kero zinazowakabili watumishi .
Alisema uwajibikaji kazini ni nguzo pekee ya ufanisi kazi hivyo kuna kila sababu ya viongozi kuwa na ushirikiano na watumishi .
“Wote  tupo sawa  na kila mmoja anafanyakazi kwenye nafasi yake ,hakuna mkubwa  zidi  ya mwenzie kwa kumfanya  mwengine  amsujudie hadi kuogopana kazini.
” Kikubwa ni kuheshimiana ,kuwa na upendo  na kuthaminiana bila kudharauliana ama kutokana na nafasi yako ya juu ndio ukandamize wengine.alisisitiza.
Nae afisa kutoka ofisi  ya waziri mkuu ,kazi,ajira,vijana na wenye  ulemavu ,Honesta  Ngolly aliyataka mabaraza ya wafanyakazi yatumie  meno yake kusimamia kero za wafanyakazi.
Alisema watumishi wana haki  ya kujiendeleza kielimu na hakuna serikali ambayo imekataza watumishi kujiendeleza.
Honesta alisema endapo watumishi watakuwa  wakiongeza elimu zao itawezesha kuongeza ufanisi makazini.
Mwenyekiti wa baraza la  wafanyakazi mkoani Pwani Edward Mwakipesile alisema mawazo na maagizo waliyopewa watayafanyia kazi ili kulinda maslahi na haki  za watumishi.
Mwakipesile aliomba ushirikiano na uwajibikaji uendelee katika mkoa huo ili kupiga hatua kutoka mkoa ulipo na kuwatumikia wananchi .
Awali kabla ya kufunguliwa baraza hilo Pascal Dawson alichaguliwa kuwa katibu  wa baraza la wafanyakazi mkoani hapo na katibu  msaidizi Asha Itelewe.

No comments:

Post a Comment