Wednesday 26 October 2016

Serikali imeanza zoezi la bomoa bomoa nyumba za biashara na makazi ya watu 110

kibam
Baadhi ya maduka Kibamba wilaya ya Ubungo yakionekana kubomolewa katika zoezi la bomoa bomoa ili kupisha upanuzi wa barabara ya kwenda Katika  ofisi za halmashauri ya wilaya ya Ubungo na hifadhi ya barabara. (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi
Serikali imeanza zoezi la bomoa bomoa nyumba za biashara na makazi ya watu 110, katika mtaa wa Kibamba halmashauri ya wilaya ya Ubungo waliojenga katika hifadhi ya barabara.
Zoezi hilo lililoanza jana ambapo linalenga kuvunja jumla ya nyumba hizo ili pia kupisha upanuzi wa barabara ya kwenda kwenye ofisi za halmashauri ya wilaya mpya ya Ubungo.
Meneja wa TANROAD  Dar es salaam, Julius Ndyamukama akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu, alisema kuwa mbali ya upanuzi wa barabara hiyo ya kwenda halmashauri , bomoa bomoa hiyo itawakumba na wale waliowekewa alama ya X na kupuuza na kuamua kuendeleza majengo yao.
Aliwashauri wananchi kutii sheria za nchi ili kuepuka adha  ya kubomolewa.
Ndyamukama aliwataka wananchi wajenge katika  maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi badala ya kujenga katika hifadhi ya barabara kama ilivyo sasa.
Baadhi ya wananchi waliokumbwa na bomoa bomoa akiwemo Adamu Mbonde, Shanifa Ngoma, Grace Lusasa , wameitupia lawama serikali kwa kushindwa kutoa notisi  ili waweze kujiandaa na kuhamisha mali zao ili zisiharibiwe.
Walisema kwanza hawajapewa notisi wala kupewa muda wa kujipanga kuhama.
Shanifa alielezea kuwa hakuna aliyekataa kuhama tatizo ni kubomolewa pasipo serikali kujali athari wanayopata wananchi ikiwemo kushindwa kutoa mabati, matofali na vifaa kutokana na tanesco kutozima umeme ili watoe mali zao.
“Tumepata hasara kubwa ya upotevu wa mali na bidhaa kwani zingine ziliharibika kutokana na kuhamisha kwa haraka na zingine ziliharibiwa na katika bomoabomoa hiyo ” alisema Shanifa.
Alifafanua kuwa wengine hawakuwekewa alama ya X lakini wamebomolewa bila taarifa wala kupewa muda kisa kupisha barabara ya kwenda ofisi za halmashauri ambayo inatumiwa pia na mkuu wa wilaya ya Ubungo.
Nae diwani wa  kata ya Kibamba Ernest Mgawe, alikiri kuwepo kwa bomoa bomoa katika kata yake lakini ameitupia lawama TANROAD kwa kushindwa kuwapa taarifa kwa maandishi na kutopewa muda.
Kwa mujibu wa diwani huyo anasema wananchi wake wamekosa muda wa kutosha wa kujiandaa hivyo sheria na taratibu zingefutwa na kujali maslahi ya wananchi.
Enerst alielezea kwamba wangearifiwa ili wahamishe mali zao bila kupata hasara.

No comments:

Post a Comment