Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usafiri Baharini Zanzibari (ZMA) Abdallah Hussein Kombo akizungumza na
waandishi wa Habari kukanusha tuhuma za kusajili Meli za Korea ya
Kaskazini kinyume na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Na Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini
Zanzibar (ZMA) imekanusha tuhuma zinazotolewa kuwa imesajili meli za
Korea Kaskazini kinyume na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa lililopitishwa mwezi Machi mwaka huu za kuzikatalia usajili
Kampuni za meli za nchi hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari, Mkurgenzi Mkuu wa ZMA Abdalla Hussein Kombo amesema tuhuma hizo
zilizotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uchambuzi wa Taasisi ya NK News
kupitia Jarida la NK Pro la Mjini Seoul, Korea Kusini sio za kweli.
Amesema ZMA baada ya kupata
taarifa ya Azimio hilo iliunda Kamati ya wataalamu kulifanyia uchambuzi
na kutoa mapendekezo kwa Mamlaka juu ya hatua za kuchukuliwa.
“Azimio hilo limetaja majina ya
meli 31 za Korea Kaskazini ambazo nchi zote wanachama wa Umoja wa
Mataifa, ikiwemo Tanzania, inazitaka kuzifutia usajili au kutozisajili,”
alisema Mkurugenzi Mkuu ZMA.
Aliongeza kuwa ZMA ilifanya
uhakiki wa meli zote zilizosajiliwa na Mamlaka hiyo na orodha ya meli
zilizoainishwa kupitia Azimio hilo na kubaini kuwa meli moja yenye jina
la First Cleam ilikuwa imesajiliwa kabla ya vikwazo vya usajili wa meli
za Korea Kaskazini lakini ikaamua kuifutia usajili.
Amesema kuanzia wakati huo,
Mamlaka haijawahi kusajili meli yeyote ambayo ilikuwemo katika orodha
iliyotolewa na Umoja wa Mataifa na imekuwa ikichukua tahadhari kubwa
katika usajili wa meli.
Mkurugenzi Mkuu wa ZMA
alisisitiza kuwa ili kuhakikisha hawatoi usajili kwa meli zenye uhusiano
na Korea Kaskazini imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Taasisi za
Kimataifa ikiwemo IMO.
Hata hivyo amekiri kuwa Kampuni
ya Filtex ambayo ilikuwa wakala wa ZMA nchini Dubai na kuvunja naye
mkataba bado inaendelea kusajili meli kwa jina la Zanzibar kinyume na
sheria.
Amesema tayari wameshawasiliana
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuifuatilia Kampuni hiyo na kuifungulia
mashtaka kwenye mahakama za Kimataifa.
Amesema katika kukabiliana na
uharamia unaofanywa na Kampuni ya Filtex, miezi michache ijayo, ZMA
itafungua Ofisi yake nchi Dubai kwa ajili ya usajili wake wa meli wa
Kimataifa.
Kufuatia majaribio ya Korea
Kaskazini kutengeneza silaha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
katika kikao chake cha 7638 kilichofanyika tarehe 2 Machi, 2016
ilipitisha Azimio la kuiongezea vikwazo Korea Kaskazini ikiwemo
kuzinyima usajili meli zote za nchi hiyo ama zenye uhusiano nazo.
No comments:
Post a Comment