Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam.
Serikali imeunda kikosi kazi
chenye wajumbe kutoka wizara sita zinazoshukulika na masuala ya ardhi
ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika kutatua changamoto mbali
mbali za ardhi ikiwemo maeneo ya Hifadhi.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaamu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhandisi Ramo Makani alisema kuwa lengo la kuhusisha Wizara hizo ni
kufanya uchunguzi wa kina na wa kisheria kuhusu namna bora na endelevu
ya kumaliza changamoto katika sekta ya ardhi.
“Serikali imeamua kuunda kikosi
kazi chenye wajumbe kutoka Wizara ya Ardhi ikiwa ni wadau wakuu, Wizara
ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Wizara ya Nishati
na Madini, Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na Wizara ya Kilimo na
Maendeleo ya Mifugo kwa madhumuni mapana ya kufanya uchunguzi wa kina na
kupitia sheria zote endelevu za kumaliza changamoto za ardhi
inayohusisha maeneo ya hifadhi” alifafanua Mhandisi Kamani
Mhandisi Makani alisema kuwa
kikosi hicho kimeanza kufanya kazi ya kusoma taarifa mbalimbali za
baadhi ya maeneo yenye changamoto za ardhi na hivi karibuni kinatarajia
kutembelea maeneo hayo ili kujua chanzo cha matatizo na jinsi ya
kushughulikia changamoto hizo.
Aidha, katika hatua hiyo ya
Serikali ya kuendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa
changamoto za ardhi, Mhandisi Makani amewataka viongozi na watumishi
wanaohusika na zoezi hilo kuzingatia taratibu katika kutekeleza sheria
kwa wananchi walioko katika vitongoji na vijiji vilivyosajiliwa.
Vilevile Mhandisi Makani
amewataka wananchi walioko katika maeneo hayo kutoanzisha shughuli mpya
za kibinadamu na kutoendelea na shughuli za kibinadamu zinazosababisha
uharibifu wa mazingira na kuathiri tabia nchi.
Wakati huohuo Mhandisi Kamani
amewataka wafugaji kuondoa haraka mifugo iliyoko ndani ya maeneo
yaliyoifadhiwa kisheria kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
Mbali na hayo Serikali imewataka
wananchi kutii sheria na kuepuka vitendo viovu vinavyosababisha kupotea
kwa uoto wa asili kwa kasi inayoendelea nchini na kutishia uhifadhi
endelevu.
No comments:
Post a Comment