Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea hundi ya shilingi 1,000,030,100/= kutoka kwa Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi (katikati) na Msajili wa Hazina,
Lawrence Mafuru (kushoto) kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi
lililotokea Kagera . Fedha hizo ni michango ya watumishi wa serikali na
Taasisi zake. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu
jijini Dar es salaam Septemba 20, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza baada ya kupokea hundi ya shilingi 1,000,030,100/= kutoka
kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi (katikati) na
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru (wapili kulia) na Msajili wa Hazina
Lawrence Mafuru (kushoto) .Fedha hizo ni michango ya watumishi wa
serikali na taasisis zake na makabidhiano yalifanyika Ofisni kwa Waziri
Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 20, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepokea jumla ya sh. bilioni 1.040 kutoka kwa watumishi na wadau
mbalimbali zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la
ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.
Makabidhiano ya michango hiyo,
yamefanyika leo mchana (Jumanne, Septemba 20, 2016) kwenye ukumbi wa
Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu,
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi alisema kiasi cha sh.
1,000,030,100 kimekusanywa kutoka kwa watumishi wa idara na Wizara zote
za Serikali na kwamba michango zaidi bado inaendelea kukusanywa.
“Tunaamini michango hii itasaidia
kuwafuta machozi wenzetu waliopatwa na maafa japokuwa tunajua
haitatosha kurudisha kile walichopoteza. Tuna imani itasaidia kupunguza
makali ya machungu waliyoyapata,” amesema.
Hata hicyo, Balozi Kijazi
amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba bado wanaendelea kukusanya michango
kutoka kwenye nyingine ambazo zilichelewa kupata taarifa na kwamba
wakikamilisha wataiwasilisha mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amepokea michango ya sh. milioni 40 na kati ya hizo, sh. milioni 20
zimetolewa na kampuni ya ujenzi ya CHICO ya China na sh. milioni 20
nyingine zimetoka kwa Umoja wa Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India
waliopo nchini (India Business Forum).
Akiwasilisha mchango wake,
Mwakilishi Mkuu wa kampuni ya CHICO hapa nchini, Bw. Guo Zhijian alisema
wamesikitishwa na maafa yaliyotokea mkoani Kagera. “Tumefanya miradi
mingi mkoani Kagera ikiwemo ujenzi wa barabara za urefu kilometa 300,
kwa hiyo mkoa huu tunaujua zaidi. Tunatoa pole kwa wote waliopatwa na
maafa hayo,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa
wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka India (IBF), Bw. Gagan Gupta
alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na kwamba
wametanguliza kiasi hicho ili kisaidie juhudi za Serikali katika
kukabiliana na maafa hayo.
“Bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wengine na tukipata michango zaidi tutaiwasilisha mapema iwezekanavyo,” amesema.
Akitoa shukrani kwa waliotoa
michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi
kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa
walengwa.
“Tunashukuru sana kwa michango
yote. Michango hii ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo.
Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na
maafa. Napenda niwahakikishie kuwa Kamati za Maafa za Mkoa, Ofisi ya
Waziri Mkuu na kamati za wilaya, ziko pale kuhakikisha walengwa
wanafikiwa,” ameongeza.
Waziri Mkuu amesema Serikali
inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi
kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa
ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.
“Ninawaomba wale walioahidi kutoa
michango wakamilishe ahadi zao na wale walio mbali na benki watumie
namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kuchangia maafa hayo,”
amesisitiza.
Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye namba 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa) au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Tetemeko hilo lililotokea
Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, lilisababisha vifo vya watu 17 na
wengine 440 kujeruhiwa. Kati yao, watu 253 walifikishwa Hospitali ya
Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38
wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji
mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia tetemeko hilo limesababisha
nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi
baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi
126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
No comments:
Post a Comment