Friday 30 September 2016

NSSF,mkoa wa Arusha,umezifikisha taasisi Nne mahakamani,kwa kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao

 Image result for nssf tanzania

Ahmed Mahmoud- Arusha

MFUKO wa hifadhi ya jamii  NSSF,mkoa  wa Arusha,umezifikisha taasisi Nne mahakama ya hakimu mkuu mkazi   Arusha,kwa kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa vipindi tofauti zaidi ya shilingi bilioni moja.
 
Mwanasheria mwandamizi wa NSSF, Selestini Ntagale, ameiambia mahakama ya hakimu mkuu mkazi kuwa taasisi hizo zimeshindwa kuwasilisha malimbikizo ya michango ya wafanyakazi hao kwenye mfuko huo licha ya kukumbushwa mara kwa mara.
 
Aliiambia mahakama hiyo kuwa michango ni haki ya mfanyakazi lakini kampuni hizo zimekuwa zikiwakata kwenye mishahara na haziwasilishi michango hiyo hivyo NSSF,kulazimika kutumia sheria kwa kuzifikisha mahakamani ili mahakama iziamuru kuwasilisha michango hiyo.
 
Miongoni mwa kampuni hizo ni pamoja na ,Water Solution, Net Health, na Hotel ya Snow Crest zote za Arusha.
 
Ntagale, aliiambia mahakama hiyo kuwa Kampuni ya Pride Tanzania, tayari ndani ya siku mbili imeshalipa shilingi milioni 180 kati ya deni lake la milioni 709 .
 
Ntagale, alisema Hotel ya Snow Crest inadaiwa tangia mwaka 2015 ambapo imechelewa kutekeleza hukumu iliyotolewa na hakimu mkazi na hivyo NSSF kukaza hukumu ambapo kama itashindwa kutekeleza NSSF itaomba kibali cha mahakama cha kuiuza  hotel hiyo kwa njia ya mnada ili kulipwa malimbikizo yanayodaiwa.
 
Aidha taasisi zingine zikiwemo Water Solution inadaiwa shilingi milioni  83.143.813,Hotel ya Snow Crest inadaiwa shilingi 449 na Net Health, inadaiwa shilingi milioni 14, 743,376,madeni ambayo ni malimbikizo  yanayotokana na makato ya mishahara ya wafanyakazi ambayo hayajawasilishwa NSSF.
 
Wakili mwandamizi, Method Kimomogoro, ambae anaiwakilisha kampuni ya Pride Tanzania, ameaiambia mahakama kuwa wateja wake wanakubaliana na deni hilo na watalilipa ndani ya mwezi mmoja .
 
Kimomogoro, aliiambia mahakama kuwa mteja wake amepewa muda mfupi wa siku mbili  na baada ya kupata taarifa hiyo wamelipa kiasi hicho cha fedha hivyo anaomba apewe muda wa mwezi mmoja hadi Novemba 4 wawe wamemaliza kiasi kilichobakia.
 
Katika hatua nyingine mahakama imetoa  hati ya kukamatwa kwa kampuni ya Net Health, ambayo haikufika mahakamani hapo huku kampuni ya Water Solution imeyakataa madai hayo ya NSSF wakidai sio sahihi .
 
Akiahirisha kesi hiyo, hakimu mkuu mkazi, Augostino Rwizila, amewataka wadaiwa wate kulipa madeni yao ndani ya muda wa mwezi mmoja ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 4 mwaka huu.
Kwenye kesi hiyo kila mdaiwa ana kesi yake binafsi  kulingana na madeni yake ingawa zote zinasikilizwa na hakimu mmoja .
 
Kesi hizo ni kama ifuatavyo, Net Health kesi namba, 389/ 2016, Pride Tanzania limited, kesi namba, 388/ 2016, Water Solution kesi namba, 390/ 2016 na Hotel ya Snow Crest kesi namba 61/ 2015 .

No comments:

Post a Comment